ACT-Wazalendo yazidi kumomonyoka

03Nov 2017
Augusta Njoji
Nipashe
ACT-Wazalendo yazidi kumomonyoka

CHAMA cha ACT-Wazalendo kimeendelea kupata pigo la viongozi na wanachama wake kukihama baada ya aliyekuwa katibu wake mkoa wa Dodoma, Weston Kaduma na wanachama 800, kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Kaduma alirudisha kadi ya chama hicho na za wanachama wengine katika uzinduzi wa kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani Kata ya Chipogoro wilayani Mpwapwa.

Alisema ameamua kujiunga na CCM baada ya kuchoshwa na siasa zilizoko ndani ya chama hicho.

 “Nimeamua kurudi huku kwa kuwa kule nilipokuwa hakuna kitu. Ndugu zangu ukiona mtu anatoka CCM… huko nje hakuna jipya, mambo yote ni ndani ya CCM,” alisema Kaduma.

Akizungumza baada ya kupokea kadi hizo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma Alhaj Adam Kimbisa, alisema Kaduma na wanachama hao wamefanya uamuzi sahihi. Aliwataka wakazi wa kata hiyo kuendeleza heshima iliyoko ya Dodoma kuwa ngome ya CCM.

Kimbisa alisema siku zote Dodoma ni ya CCM, hivyo watumie uchaguzi huo kumpa Rais John Magufuli nguvu kwa kumchagua Hosea Fweda.

“Juzi kuna chama kilikuja kuzindua kampeni zake hapa. Kuna vijana walienda, nawapongeza vijana wale kwa kwenda kuwapa kampani, lakini nina uhakika ndani ya mioyo yao wanasema wataipigia kura CCM, maana ndugu zangu mgeni akija kwako ukimuacha peke yake hatajisikia vizuri,”alisema Kimbisa.

Naye Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde, aliwataka wakazi wa Chipogoro kuimarisha umoja wao, kuepuka vurugu, kushauriana, kubishana kwa hoja na kumchagua diwani anayetokana na CCM ambaye ni Fweda.

“Ndugu zangu mchagueni Hosea atetee shida zenu, awasilishe shida zenu kwa tajiri… ukimchagua Hosea awe diwani wa kata hii kwa tiketi ya CCM atapiga mpira utapokelewa na mbunge, mbunge naye atapiga shuti kali mpaka golini ambapo ni kwa rais,” alisema Lusinde.

Kwa upande wake, Fweda aliwaomba wananchi wamchague ili ashirikiane nao katika kuwaletea maendeleo na kuahidi kuwa diwani wa Chipogoro katika kuwatumikia.

Habari Kubwa