ACT yaijibu CCM ubunge wa Zitto

26May 2020
Enock Charles
Dar es Salaam
Nipashe
ACT yaijibu CCM ubunge wa Zitto

HATIMAYE Chama cha ACT-Wazalendo, kimeijibu hoja ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Humprey Polepole, kwamba Zitto Kabwe hatarejea bungeni baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Mkuu wa ACT-Wazalendo, Ado Shaibu, picha mtandao

Mara kadhaa Polepole amenukuliwa akitoa kauli ya kumtaka Kiongozi Mkuu huyo wa ACT-Wazalendo (Zitto) atafute kazi nyingine ya kufanya kwa kuwa ana uhakika hatashinda kiti cha ubunge katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.

Zitto (43), kwa sasa ni Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo) na kabla ya hapo, alikuwa Mbunge wa Kigoma Kusini (Chadema). Mwanasiasa huyo pia aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC).

Wiki iliyopita, Nipashe ilipata nafasi ya kuzungumza kwa faragha jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo, Ado Shaibu, ambaye pamoja na mambo mengine, alijibu hoja hiyo ya Polepole.

Shaibu alimkumbusha Polepole kuwa kuna tatizo la uhaba wa ajira nchini ambalo ni silaha tosha kwa ACT-Wazalendo na vyama vingine vya upinzani kuitumia wakati wa kampeni kuiharibia kura CCM.

Kiongozi huyo wa ACT-Wazalendo pia alikumbusha kilio cha watumishi wa umma kuhusu kutopandishwa madaraja na kupewa nyongeza ya mishahara.

Ifuatayo ni sehemu ya mazungumzo ya Nipashe na kiongozi huyo wa ACT-Wazalendo:

SWALI: Kwa hali ilivyo sasa kisiasa nchi, ACT-Wazalendo ina matumaini ya kuwa na uwakilishi bungeni na hata kushinda nafasi ya urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu?

SHAIBU: Kwanza vyama vya upinzani vinao wajibu wa kufikisha ujumbe mahususi kwa umma kwamba mchakato wa uchaguzi hauna maana ni mchakato wa madaraka pekee; kwamba tunachagua wabunge, madiwani, wawakilishi pamoja na Rais. Una maana kubwa pia katika maisha yao.

Hili ndiyo tunalopaswa kulifikisha, kwamba kwa wafanyakazi wa Tanzania ambao hawajapata nyongeza ya mishahara kwa miaka mitano yote ya serikali hii, wafahamu kuna uhusiano wa moja kwa moja baina ya mchakato wa uchaguzi na hali inayowakumba kwa wafanyabiashara ndogondogo na wawekezaji wakubwa ambao biashara zao zimeathirika kutokana na vyuma kukaza.

Wafahamu uhusiano wa moja kwa moja yaliyokuwapo baina ya ufanisi wa biashara zao na uchaguzi wa mwaka 2020, kwa vijana kukosa ajira, vijana wa vyuo vikuu waliokosa mikopo, waandishi wa habari ambao haki zao zimebinywa.

Kwa kila Mtanzania ambaye anaona hali ya maisha imebadilika, auone uchaguzi huu kuwa una maana kubwa katika maisha yake. Kwa hiyo, hii ndiyo kazi kubwa tunayokwenda kufanya kuwavutia wananchi waweze kushiriki katika uchaguzi.

Iwapo wananchi wanautazama uchaguzi huu kama tu uchaguzi wa kuchagua mbunge, diwani na Rais, basi eeeh hawatokuja, lakini wananchi somo likiwaingia kuwa huu ni uchaguzi wao unaohusu maisha yao, unaohusu mustakabali wao, tuna uhakika kwamba wataweza kuisusia CCM.

SWALI: Mara kadhaa umeshamsikia Polepole akitamka wazi kuwa Zitto hatarejea bungeni? Hili unalizungumziaje?

SHAIBU: Linapokuja suala kwamba kuna ubabe unaotumika kuhakikisha CCM inashinda, kwa uzoefu tulioupata kutoka katika uchaguzi wa marudio na uchaguzi wa serikali za mitaa, kazi ya upinzani ni 'ku-mobilize' umma.

Ukiona maovu yanafanyika, umma hauchukui hatua maana yake upinzani, wanaharakati na mawakala wengine wa mabadiliko hawajauhamasisha umma vya kutosha, ili uweze kuchukua hatua.

Lakini sisi si wajinga ya kwamba kilichotokea kwenye uchaguzi wa marudio kimetokea, kilichotokea kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa kimetokea, basi tutakwenda uchaguzi mkuu hivyo hivyo.

Ipo kazi kubwa inaendelea kufanywa na itaendelea kufanywa wakati wa kampeni kuhakikisha kwamba yaliyojitokeza nyuma hayajitokezi tena.

Hatuwezi kutaja tunajipanga vipi kimkakati, lakini kazi kubwa inaendelea kufanywa kuhakikisha kwamba basi umma unashinda katika uchaguzi mkuu huu wa 2020.

Habari Kubwa