ACT yaonya nchi bila viongozi

14May 2018
Gwamaka Alipipi
DAR ES SALAAM
Nipashe
ACT yaonya nchi bila viongozi

CHAMA cha ACT-Wazalendo kimesema uamuzi wa serikali kupiga marufuku wanafunzi wa vyuo vikuu nchini kujihusisha na siasa kutaicha nchi bila ya viongozi wake wa baadaye.

Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mawasiliano kwa Umma wa ACT, Ado Shaibu.

ACT imesema viongozi wa kitaifa wanaoongoza nchi kwa sasa na wastaafu walijenga uwezo wao tangu wakisoma vyuoni.

Hayo yalisemwa jana na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mawasiliano kwa Umma wa ACT, Ado Shaibu wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uamuzi wa Rais John Magufuli kupiga marufuku wanafunzi vyuo vikuu kujihusisha na siasa wanapokuwa vyuoni.

Rais Magufuli, akiwa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) mjini Morogoro wiki iliyopita, aliwataka wanafunzi wa vyuo vikuu kutovigeuza sehemu ya kufanya siasa, bali yawe maeneo ya kusoma na kufanya tafiti.

“Wanangu, vijana wangu msiende kwenye direction (mwelekeo) huo," alisema Rais Magufuli. "Timizeni wajibu wenu, someni, yale mengine mtayakuta".

"Siasa mtazikuta na mtazikimbia wenyewe, msiingie kwenye mikumbo, kila mtu anajua maisha ya familia aliyotoka.

"Pasua misonge (tafuteni alama A).”

Pia Rais Magufuli aliwataka wanafunzi hao kutofanya vurugu vyuoni, na kuwaeleza kuwa kwa yeyote atakayefanya fujo hatasita kumfukuza.

Akizungumzia kauli hiyo, Shaibu alisema vyuo vikuu ndiyo sehemu inayowajenga vijana wa baadaye wenye uwezo wa kujenga hoja na kuongoza nchi.

Shaibu alisema viongozi wa nchi kama vile Jaji Joseph Warioba, Rais mstaafu Jakaya Kikwete, marehemu Samuel Sitta na wengineo wengi uwezo wao wa kuongoza nchi ulijengwa tangu wakiwa wanasoma vyuoni.

“Mwaka 1965 Jaji Warioba alikuwa mwenyekiti wa wanafunzi wa vyuo vikuu Tanganyika, viongozi wengi waliopo madarakani uwezo wao ulijengwa na vyuo vikuu, kuzuia siasa vyuoni siyo sawa,” alisema Shaibu.

Naye Mwenyekiti wa ngome ya vijana wa ACT-Wazalendo, Likapo Likapo alisema Rais Magufuli anawajibu wa kuwalinda na kuwaendeleza vijana kisiasa ili wawe viongozi wazuri waweze kuongoza nchi.

“Tunamuomba Rais Magufuli atafakari upya kauli hiyo, ili vijana waweze kujijenga vizuri kwa maslahi ya taifa,” alisema Likapo.

Alisema hakuna chuo chochote nchini kinachoruhusu siasa lakini kuna utaratibu uliowekwa katika vyuo hivyo wa kuwawezesha wanafunzi kufanya siasa.

Alisema vijana wa vyuo vikuu nchini wana wajibu wa kushindana na vijana wa vyuo vikuu vingine katika masuala ya siasa, uchumi, kimaendeleo na kijamii.