ACT yataka CAG akague pato tozo miamala simu

17Jun 2022
Moshi Lusonzo
DAR ES SALAAM
Nipashe
ACT yataka CAG akague pato tozo miamala simu

CHAMA cha ACT-Wazalendo kimemshauri Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya ukaguzi maalum wa matumizi ya fedha zote zilizopatikana kutokana na tozo za miamala ya simu baada ya kuwapo kwa kile kilichodai mkanganyiko wa matumizi yake.

Msemaji wa Sekta ya Fedha wa chama hicho, Emmanuel Mvula.

Pia kimeitaka serikali kuwachukulia hatua watu wote waliohusika na hasara ya Sh. bilioni 208 katika zao la korosho mwaka 2018.

Msemaji wa Sekta ya Fedha wa chama hicho, Emmanuel Mvula, alitoa rai hiyo jana jijini wakati akitoa tathmini ya uchambuzi wa bajeti ya serikali inayopendekezwa kwa mwaka 2022/23.

Mvula alisema jumla ya Sh. bilioni 261 zilizokusanywa kuanzia mwezi Julai 2021 hadi Machi 2022, sawa na asilimia 25.6 ya lengo ya makadirio ya trilioni 1.02, zimekuwa na mkanganyiko wa matumizi kutokana na miradi lengwa kutekelezwa na fedha za mkopo wa serikali wa kuimarisha uchumi kutokana na athari za ugonjwa wa Uviko-19 uliotolewa na Shirika la Fedha Duniani (IMF).

Alisema awali ACT-Wazalendo walitahadharisha kuanzishwa kwa tozo hizo kutaongeza maumivu makubwa kwa wananchi.

“Tunamshauri CAG kufanya ukaguzi maalum katika matumizi ya fedha hizi za tozo za simu kwa sababu kuna mkanganyiko mkubwa wa matumizi kutokana na ujio wa mkopo wa Uviko-19," alisema Mvula.

Alisema chama hicho pia kinaitaka serikali kufuta kabisa tozo hiyo na irudi kama ilivyokuwa kabla ya mwezi Julai mwaka 2021 ili kuwapunguzia mzigo wananchi.

Kuhusu korosho, Mvula alisema chama chake kinaitaka serikali kuwachukulia hatua wale wote waliohusika kupata hasara kutokana na kuingilia soko la zao hilo.

Alisema ili kutekeleza hatua ya serikali kununua korosho kwa wakulima, Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) ilikopa Sh. bilioni 208 kwa ajili ya ununuzi baada ya watu binafsi kupigwa marufuku kununua korosho.

“Katika Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 iliyosomwa bungeni, Waziri wa Fedha ametangaza serikali kulibeba deni hilo, lakini wahusika waliosababisha hasara hiyo wapo na haijaelezwa wanafanywa nini, tunataka uwazi na uwajibikaji kufuatia uamuzi huo,” alisisitiza.

Mvula alisema katika mapendekezo yao wanaitaka serikali kurudisha mapato yanayotokana na ushuru wa mauzo ya nje ya korosho ghafi ambayo wamechukua tangu mwaka 2018.

“Kabla ya mabadiliko, asilimia 65 ya mapato yatokanayo na ushuru wa mauzo ya nje yanarudi kwa wakulima kupitia mfuko wa kuendeleza zao la korosho, hivyo ni muhimu kurudisha kwa ajili ya kuongeza kiwango cha uzalishaji," alisema.

Katika uchambuzi wake, chama hicho kimegusia Deni la Taifa kikiishauri serikali kuachana na mikopo yenye masharti magumu ya kibiashara, pia kimegusa mgawanyo wa fedha za Muungano huku kikitaka waajiri na wafanyakazi wapunguziwe kilichokiita mzigo wa kodi katika mishahara.

Habari Kubwa