ACT yatamba ‘kunyakua’ majimbo Tunduru

25Sep 2020
Stephen Chidiye
Tunduru
Nipashe
ACT yatamba ‘kunyakua’ majimbo Tunduru

CHAMA cha ACT-Wazalendo wilayani hapa kimetamba kupata ushindi wa kishindo kwenye majimbo ya Tunduru Kaskazini na Kusini katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28, mwaka huu.

Katibu Mkuu wa chama hicho taifa na mgombea ubunge wa Jimbo la Tunduru Kaskazini, Ado Shaibu, alisema hayo wakati akiongea na wananchi waliojitokeza kwenye mapokezi ya wagombea wa chama hicho yaliyofanyika Kijiji cha Sisikwasisi hadi makao makuu ya chama hicho Tunduru Mjini.

Akifafanua taarifa hiyo, Shaibu alisema wingi wa wananchi waliojitokeza katika mapokezi hayo kunaonyesha kukubalika kwa wagombea walioteuliwa kupeperusha bendera ya chama hicho katika majimbo ya Tunduru Kusini linalowaniwa na Mtutura Abdalah Mtutura na Ado Shaibu wa Tunduru Kaskazini.

Mgombea wa chama hicho katika Jimbo la Tunduru Kusini, Mtutura, alisema mapingamizi ya CCM yaliyowekwa dhidi yao yalilenga kuwasaidia wagombea wa chama hicho kupita kwa mtelezo hivyo ushindi kwenye majimbo yote kwa ACT-Wazalendo upo wazi.

Alisema baada ya kuwekewa mapingamizi hayo, waliamua kwenda jijini Dar es Salaam na kuandika rufani ambazo zimewashawishi viongozi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kurudisha majina yao ili waingie kwenye kinyang’anyiro hicho hatua inayo wahakikishia kuibuka na ushindi kupitia sanduku la uchaguzi Oktoba 28.

Awali, Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, Wilaya ya Tunduru, Mohammed Mawila, aliwaeleza wananchi hao kuwa watarajie kampeni za ustaarabu katika kipindi chote cha kampeni na kwamba siku ya uzinduzi watakuwapo viongozi wa kitaifa wa chama hicho na watashiriki kwa kubadilishana hadi mwisho wa kampeni hizo kwa ajili ya kuwanadi wagombea wa nafasi za urais, ubunge na udiwani.

Habari Kubwa