ACT yatoa kauli Membe kujivua uanachama

03Jan 2021
Enock Charles
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
ACT yatoa kauli Membe kujivua uanachama

ALIYEKUWA mgombea urais kupitia Chama cha ACT-Wazalendo, Bernard Membe, amejivua uanachama wake na nafasi yake ya mshauri mkuu wa chama hicho, ikiwa ni takribani siku 170 tangu ajiunge nacho Julai 16, mwaka jana.

Waziri huyo wa zamani wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, alitangaza uamuzi huo juzi usiku, akibainisha kuwa kwa sasa, atakuwa mshauri wa masuala mbalimbali yanayoihusu nchi na kupigania demokrasia ya kweli.

Akizungumzia uamuzi huo wa Membe, Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo, Ado Shaibu, aliiambia Nipashe jana kuwa chama hicho kilikuwa na taarifa za kusudio hilo la Membe kwa muda mrefu na kwamba kinamtakia heri huko aendako.

Shaibu alisema chama hicho hakina kinyongo na uamuzi huo na kamwe hakitajiingiza kwenye malumbano na mwanasiasa huyo, ambaye kabla ya kujiunga nacho, alifukuzwa uanachama ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

"Taarifa hizi za ndugu Membe kujiuzulu uanachama wa chama chetu na kujivua nafasi zote za uongozi tumezipokea na kimsingi siyo taarifa ngeni kwa sababu tumekuwa tukizifahamu. Ndugu Membe mwenyewe amewasiliana na sisi mara kadhaa.

"Hata baada ya Uchaguzi Mkuu, Ndugu Membe ilikuwa ni kana kwamba ameshajiweka pembeni na shughuli za chama.

"Tunachoweza kusema kama chama ni kwamba, sisi ACT-Wazalendo tunao utamaduni wa muda mrefu, mtu yeyote akijiondosha kwenye chama, mara nyingi tunajiepusha na malumbano na tunamtakia kila la heri," Shaibu alisema.

Membe alijiunga na ACT-Wazalendo Julai mwaka jana, baada ya kuvuliwa uanachama wa CCM Februari mwaka jana, akituhumiwa kukiuka maadili ya chama hicho...soma zaidi kupitia https://epaper.ippmedia.com

 

Habari Kubwa