Adaiwa kuchoma nyumba ya jirani, naye achomwa

03Oct 2021
Idda Mushi
Morogoro
Nipashe Jumapili
Adaiwa kuchoma nyumba ya jirani, naye achomwa

​​​​​​​MKAZI wa Kijiji cha Dakawa, Kata ya Bwakila Chini, Juma Katinda (58), ameuawa na kundi la watu wenye hasira kali ikidaiwa ni kulipiza kisasi baada ya kutuhumiwa kuchoma moto nyumba ya jirani yake.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Fortunatus Muslim.

Kutokana na tukio hilo la mauaji, watu 20 wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa ajili ya uchunguzi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Fortunatus Muslim, alisema jana kuwa mauaji hayo yalitokea Septemba 29, mwaka huu saa 11 jioni katika maeneo ya Kitongoji cha Mgamba, Kijiji cha Dakawa katika Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro.

Alibainisha kuwa kutoka na tukio hilo, msako wa jeshi hilo ulifanywa na kufanikisha kutiwa mbaroni kwa watu 20 wakituhumiwa kuhusika na mauaji hayo kwa kujichukulia sheria mkononi, wakiwamo wanane waliokamatwa ndani ya basi katika harakati za kutoroka kijijini huko.

Kamanda Musilim alisema watuhumiwa hao wanadaiwa kumshambulia Katinda kwa kumpiga na kumsababishia kifo na baadaye kuuteketeza mwili wake kwa moto umbali wa mita 200 kutoka eneo ambalo alidaiwa kuchoma nyumba.

Awali, ilidaiwa kuwa Katinda alichoma moto nyumba ya jirani yake aliyetajwa kwa jina moja la Ruchamla kwa madai kuwa eneo ilikojengwa nyumba hiyo ni lake na ilijengwa wakati akiwa safarini kwa muda mrefu.

"Awali wananchi walijitokeza kwenda kutoa msaada wa kuzima moto nyumba iliyochomwa lakini Katinda aliwazuia wasitoe msaada ndipo wananchi wakaitana kwa wingi na kumzingira kisha kumshambulia kwa silaha za jadi na kumuua na mwili kuuteketeza kwa moto," alidai Kamanda Musilim.

Kiongozi huyo wa Jeshi la Polisi aliitembelea familia ya mwenye nyumba iliyochomwa moto na kuwapa pole pamoja na familia ya marehemu iliyookolewa wakiwamo wake zake watatu, watoto, ndugu na jamaa wanaofikia 11 waliopelekwa kuhifadhiwa Kituo cha Polisi Duthumi kwa ajili ya usalama wao.

Katika mkutano na wananchi wa Kata ya Bwakila Chini ambao ulihudhuliwa na viongozi mbalimbali wa kijiji hicho, Kamanda Musilim aliwataka wananchi kuachana na vitendo vya kujichukulia sheria mikononi badala yake watoe taarifa kwenye vyombo vya dola kuhusu matukio yoyote ya kiuhalifu.

Habari Kubwa