Adaiwa kujinyonga kisa deni la benki

24Jan 2021
Christina Haule
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Adaiwa kujinyonga kisa deni la benki

WATU sita wamefariki dunia katika matukio tofauti mkoani Morogoro, yakiwamo ya kufa maji na kudaiwa kujinyonga huku mtu mmoja akinusurika kupoteza maisha baada ya kudaiwa kujaribu kujiua kwa kunywa sumu ya kuhifadhia mahindi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Fortunatus Musilimu, aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa, tukio la kwanza lilitokea Januari 13 majira ya saa 10 jioni kijijini Mmgeta wilayani  Kilombero, linamhusu kijana Felisian Mwampinzi (22).

Mkulima huyo na mkazi wa Mngeta, alikutwa akiwa amefariki dunia akidaiwa kujinyonga ndani ya chumba chake kwa kutumia nguo ya kitenge huku chanzo cha kuchukua uamuzi huo kutokana na ujumbe unaodaiwa aliuacha, kwamba ameamua kujinyonga kwa kuwa anadaiwa na benki.

Kamanda Muslimu alisema katika ujumbe huo, marehemu alidai alikopa deni kwa ajili ya mama yake lakini mama yake amekataa kulilipa, hivyo anasumbuliwa na benki na ndiyo sababu ya kuamua kujinyonga ili asisumbuliwe tena.

Hata hivyo, kiongozi huyo wa Jeshi la Polisi alisema wakati kijana huyo anajinyonga, hakukuwa na mtu yeyote   nyumbani  na mwili wake ulihifanyiwa kwa ajili ya uchunguzi na baadaye ukakabidhiwa kwa ndugu zake kuendelea na taratibu za maziko. 

Katika tukio la pili, Jafary Isaka (28), mkulima na mkazi wa Kijiji cha Mkula B, amekutwa akiwa amefariki dunia baada kudaiwa kujinyonga kwa kutumia kamba aliyoitengeneza kwa kuchana shuka na kuifunga kwenye moja ya kenchi ndani ya chumba chake.

Kamanda Musilimu alisema tukio hilo lilitokea mnamo Januari 16 majira ya saa 10 jioni katika maeneo ya Mkula B, Kata ya Mkula, wilayani Kilombero ambapo chanzo cha tukio hilo bado hakijafahamika kwa kuwa hakuna ujumbe wowote ulioachwa na kijana huyo.

Alisema mwili wa kijana huyo umefanyiwa uchunguzi na daktari na kukabidhiwa kwa ndugu kwa taratibu za mazishi.

Katika tukio la tatu, Cecilia Ching'unyau (22), mkulima na mkazi wa Magoweko, Tarafa na Wilaya ya Gairo, amenusurika kufa baada ya kudaiwa kujaribu kujiua kwa kunywa sumu ya kuhifadhia mahindi.

Kamanda Musilimu alisema tukio hilo lilitokea Januari 14, mwaka huu majira ya saa moja usiku katika Mtaa wa Magoweko ambapo mtuhumiwa anadaiwa kunywa sumu ya kuhifadhia mahindi aina ya Acteric kwa kuchanganya na pombe aina ya vodka-cuca.

Alisema alikutwa akiwa amelewa na kupoteza kumbukumbu huku akiwa ameegemea  ukuta wa nyumba na pembeni yake kulikutwa makopo mawili vya pombe hiyo yakiwa yameshatumika na makopo mawili vyenye sumu hiyo.

Alisema mtuhumiwa amelazwa Kituo cha Afya Gairo akiendelea na matibabu na hali yake inaendelea vizuri, akidai kuwa chanzo cha tukio ni wivu wa kimapenzi kuwa wazazi wanaingilia kuvunja uhusiano na mpenzi wake. 

Katika tukio la nne lililotokea Kijiji cha Mbasa, Tarafa ya Ifakara, Kilombero, mwili wa Msham Abdalah (21), mkulima na mkazi wa Kapolo, uliokotwa ukielea katika Mto Kikwawila.

Kamanda Muslimu alisema mwili huo ulikutwa ukielea kwenye mto huo huku chanzo kikidaiwa huenda alishindwa kuvuka kutokana na maji ya mvua kujaa kwenye mto huo.

Katika tukio la sita, lililotokea Kitongoji cha Zambia, Kijiji cha Biro wilayani  Malinyi, limehusisha vifo vya watoto wawili wa kike; Ester Zakayo (9) na Ester Malechela (10), wote wakiwa ni wanafunzi wa darasa la pili katika Shule ya Msingi Biro.

Wanafunzi hao wanadaiwa kufa maji wakati wakiogelea kwenye dimbwi la maji.

Kamanda Muslimu alisema watoto hao walifariki dunia baada ya kuzama kwenye dimbwi la maji walipokuwa wakicheza kutokana na mvua  zinazoendelea kunyesha.

Wakati huo huo, Samwel Lifa (24), mkazi wa Kijiji cha Msimba, Tarafa ya Mikumi wilayani Kilosa, anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kumbaka na kumtia mimba mwanafunzi wa  kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari Mikumi Day.

Kwa mujibu wa Kamanda Muslimu, kijana huyo alikamatawa Januari 19 majira ya saa sita katika maeneo ya Kijiji cha Msimba.

Habari Kubwa