Adaiwa kujiua kisa madeni

06Jul 2019
Beatrice Moses
Nipashe
Adaiwa kujiua kisa madeni

MWANAMUME aliyetambulika kwa jina la Evarist Massawe,  anadaiwa kujiua na kuacha ujumbe akielezea sababu za kuchukua uamuzi huo kuwa ni kutapeliwa Sh.  milioni sita na kujikuta akielemewa na madeni. 

Massawe, alikuwa mgane, alikuwa mfanyabiashara na mkazi wa mtaa wa Ukombozi, Kata ya Saranga, Ubungo jijini Dar es Salaam.

Baadhi ya mashuhuda walisema Massawe alijiua  siku kadhaa zilizopita bila kugundulika hadi harufu kali ilipojitokeza juzi na kushtua majirani zake. 

Akizungumza na Nipashe, Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Ukombozi, Yessaya Mande, alisema alipigiwa simu juzi saa moja usiku alipokuwa amejipunzisha nyumbani kwake na baada ya kufika eneo la tukio, alibaini kwamba kuna mtu amekufa. 

"Niliambiwa niingie ndani ya nyumba ya Massawe ili nijue kuna tatizo gani. Baada ya kuingia, nilikuta harufu kali na nilipotazama vizuri niliona mwili wake ukiwa umevimba na kuna damu zimesambaa hali ilikuwa inatisha nikatoka haraka kule chumbani," alisema Mande. 

Alisema polisi walipewa taarifa na walifika na kuingia kwenye nyumba hiyo kisha baada ya kusogeza mwili ili kuuondoa ndipo walipoona barua ambayo inasadikiwa kuwa iliandikwa na Massawe kabla ya kujiua. 

" Katika barua ile aliandika mambo mengi lakini alieleza kuwa uamuzi wake wa kujiua unatokana na kudhulumiwa  Sh. milioni sita na wakala wa Vodacom aliyemtaja kwa jina la Raphael, wakati yeye ana madeni mengi ikiwamo kudaiwa na benki na watu binafsi," alisema Mande. 

Alisema kuwa Massawe katika barua yake hiyo alidai kwamba kuna mtu anayemdai Sh.  200,000 ambaye amekuwa akimsumbua ambaye hakuwa akiamini kuwa kuna mahali alikuwa akidai fedha ambazo ametapeliwa. 

"Pia pamoja na maelezo mengine, Massawe aliagiza mwili wake usisafirishwe kwenda kuzikwa kwao Rombo mkoani Kilimanjaro, bali azikwe kwenye makaburi ya hapa Saranga," alisema Mande.  

Baadhi ya majirani ambao hawakuwa tayari majina yao kutajwa kwenye gazeti,  walieleza kwa nyakati tofauti kuwa Massawe alikuwa na wakati mgumu hasa baada ya mkewe kufariki dunia  miaka kadhaa iliyopita, hivyo alikuwa na maisha ya upweke. 

Kamanda wa Polisi Kinondoni, Mussa Taibu, akizungumza na gazeti hili alisema bado hajapata taarifa rasmi kuhusu tukio hilo, hivyo akaahidi kulifuatilia.