Adaiwa kumuua mtoto wake kwa kumkatakata na shoka

16Sep 2021
Elizabeth John
NJOMBE
Nipashe
Adaiwa kumuua mtoto wake kwa kumkatakata na shoka

VIOLET Chaula (30) mkazi wa kijiji cha Mkongomi, Kata ya Kidugala, Wanging’ombe mkoani Njombe, anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kumuua mtoto wake wa kumzaa, Azgad Kinyunyu (3) kwa kumkatakata na shoka kichwani.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Hamisi Issah

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Hamisi Issah, alisema kwa mujibu wa maelezo ya wanandugu mwanamke huyo alikuwa na matatizo ya akili.

Alisema miezi michache iliyopita, mwanamke huyo akiwa mjini Makambako alikokuwa ameolewa, alipatwa na matatizo ya akili na kurudishwa nyumbani  kwa wazazi wake ili apatiwe matibabu.

Kamanda alisema akiwa na mtoto huyo ambaye alionekana kudeka, mama yake huyo aliona kuwa ni usumbufu, hivyo alichukua shoka ili kumkata kata.

"Huo ni ukatili tunaita ingawa huyu mama ni mgonjwa. Lakini  sasa sheria haisemi namna hiyo," alisema Issah.

Alisema mwanamke huyo anashikiliwa na jeshi hilo na wanasubiri kukamilika kwa baadhi ya ushahidi ili afikishwe mahakaman.

Wakati huo huo, mwanafunzi wa kidato cha sita Shule ya Sekondari Mwakavuta, wilayani Makete, Ndenja Ng'wale, amejinyonga kwa kutumia kamba za manila katika mtaa wa SIDO Njombe mjini.

Kamanda Issah alisema mwanafunzi huyo alirudi nyumbani kwa ruhusa kutoka shule aliyokuwa anasoma kutokana na kuumwa jino.

Alisema alikwenda kwa shangazi yake kwa lengo la kupata matibabu, lakini katika hali isiyo ya kawaida, kijana huyo alipona jino na kuanza kuumwa na tumbo huku akitapika.

"Hapo kijana hata hatujui msongo wa namna gani ulimpata kwani alichukua sturi na kamba ya manila na kujinyonga kwenye kenchi ya nyumba hiyo hadi kufa," alisema Issah.

Alisema matukio ya kujinyonga hadi kufa familia zinapaswa kuwaangalia watu wao na kuwapa ushauri nasaha ili wasifanye vitendo hivyo.