Adaiwa kuua dada kumkuta na mpenzi wake nyumbani

15Jul 2019
Na Mwandishi Wetu
KAHAMA
Nipashe
Adaiwa kuua dada kumkuta na mpenzi wake nyumbani

JESHI la Polisi mkoani Shinyanga linamtafuta Daudi Bundala kwa tuhuma za kumshambulia dada yake, Suzana Bundala (21), kwa kumpiga kitu kizito kichwani na kumsababishia kifo, baada ya kumkuta akiwa amelala na mpenzi wake nyumbani kwao.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Richard Abwao.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Richard Abwao, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema lilitokea Ijumaa usiku katika Kijiji cha Bugoshi, Kata ya Uyogo Wilaya ya Kipolisi Ushetu.

Alisema kuwa, chanzo cha tukio hilo ni Suzana kukutwa akiwa na mpenzi wake, Eddy Nkimbila, nyumbani kwao kitendo kilichomchukiza mtuhumiwa na kumshambulia dada yake na kumsababishia kifo.

“Ilikuwa saa tano kamili usiku katika Kijiji cha Bugoshi ambapo Daudi Bundala alimkuta dada yake akiwa amelala na mpenzi wake Eddy Nkimbila nyumbani kwao kisha kumshambulia na kitu kizito kichwani na kumsababishia kifo,” alisema Kamanda Abwao.

Kamanda Abwao alisema hata hivyo, mtuhumiwa akimbia baada ya tukio hilo na juhudi za kumtafuta na kumkamata zinaendelea, na kuongeza kuwa mwili wa marehemu umekabidhiwa kwa ndugu zake kwa ajili ya taratibu za mazishi.

Aliwataka wananchi mkoani Shinyanga kuacha tabia ya kuendelea kujichukulia sheria mkononi, ili kuepisha matukio ya kikatili na uvunjaji wa sheria.