Adengenye RC Kigoma, Mwanri astaafu Tabora

04Jul 2020
Mary Geofrey
Dar es Salaam
Nipashe
Adengenye RC Kigoma, Mwanri astaafu Tabora

RAIS John Magufuli amefanya uteuzi wa wakuu wa mikoa miwili, akimteua aliyekuwa Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Thobias Andengenye, kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kigoma kuchukua nafasi ya Brigedia Jenerali mstaafu Emmanuel Maganga ambaye amestaafu.

Aliyekuwa Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Thobias Andengenye, ambaye sasa ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kigoma:PICHA NA MTANDAO

Januari 23, mwaka huu, Rais Magufuli alitengua uteuzi wa Andengenye na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, kutokana na mkataba mbovu ambao jeshi hilo liliingia na Kampuni ya Romania kwa ajili ya ununuzi wa vifaa mbalimbali.

Hata hivyo, mapema mwezi uliopita, Rais Magufuli  wakati akizindua Jengo la Jeshi la Magereza mkoani Dodoma, alitangaza kumsamehe Andengenye kwa maelezo kuwa kiongozi huyo alikuwa akimwomba msamaha mara kadhaa.

Rais Magufuli alitangaza uteuzi huo jana jijini Dodoma, akiteua pia wakuu wa wilaya tisa nchini ambao wanatarajiwa Jumatatu Julai 6 mwaka huu.

Katika taarifa iliyotolewa jana na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa, Rais Magufuli amemteua Dk. Philemon Sengati kuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora.

Dk. Sagati ambaye alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Magu mkoani Mwanza, anachukua nafasi ya Aggrey Mwanri ambaye amestaafu.

Kuhusu wakuu wa wilaya tisa, taarifa hiyo ilieleza kuwa, Rais Magufuli amemteua Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza Ismail Mlawa, kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro.

Kabla ya uteuzi huo, Mlawa alikuwa Mkuu wa Magereza wa Mkoa wa Morogoro na amechukua nafasi ya James Ihunyo ambaye amestaafu.

Taarifa hiyo ilieleza zaidi kuwa, Rais Magufuli amemteua Jamila Yusuf kuwa Mkuu wa Wilaya ya Mpanda mkoani Katavi. Kabla ya uteuzi huo, Jamila alikuwa Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dodoma na anachukua nafasi ya Lilian Matinga ambaye amestaafu.

Rais Magufuli pia amemteua Martine Ntemo kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kibaha mkoani Pwani. Awali alikuwa Mhandisi katika Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na anachukua nafasi ya Asumpter Mshama ambaye amestaafu.

Vilevile, Rais Magufuli amemteua Salum Kali kuwa Mkuu wa Wilaya ya Magu mkoani Mwanza, ambaye kabla ya uteuzi, alikuwa Katibu wa CCM Mkoa wa Mwanza na anachukua nafasi ya Dk. Philemon Sengati ambaye ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora.

Mwingine aliyeteuliwa ni Wilson Shimo ambaye anakuwa Mkuu wa Wilaya ya Nyang’wale mkoani Geita. Kabla ya uteuzi huo, alikuwa Katibu Tawala wa Wilaya ya Singida.

Rais Magufuli pia amemteua Kanali Mathias Kahabi, kuwa Mkuu wa Wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera, akichukua nafasi ya Saada Malunde ambaye amestaafu.

Taarifa hiyo pia ilieleza kuwa, Rais Magufuli amemteua Abbas Kayanda kuwa Mkuu wa Wilaya ya Karatu mkoani Arusha. Kabla ya uteuzi, alikuwa Katibu Tawala wa Wilaya ya Karatu na anachukua nafasi ya Theresia Mahongo ambaye amestaafu.

Uteuzi mwingine ni wa Lazaro Twange ambaye anakuwa Mkuu wa Wilaya ya Babati mkoani Manyara. Twange anachukua nafasi ya Elizabeth Kitundu ambaye amestaafu.

Rais Magufuli pia amemteua Toba Nguvila kuwa Mkuu wa Wilaya ya Handeni. Kabla ya uteuzi, alikuwa Katibu Tawala wa Wilaya ya Longido mkoani Arusha.

Nguvila anachukua nafasi ya Godwin Gondwe ambaye amehamishwa kituo cha kazi na kuwa Mkuu wa Wilaya ya Temeke mkoani Dar es Salaam, kuchukua nafasi ya Felix Jackson aliyestaafu.

“Uteuzi wa viongozi hao umeanza leo (jana) Julai 3, mwaka huu na wateule wote wanatakiwa kuwapo Ikulu, Chamwino mkoani Dodoma Julai 6 saa 4:00 asubuhi," ilielezwa katika taarifa hiyo ya Ikulu.

Habari Kubwa