Adha mwendokasi sasa kuwa historia

22Oct 2018
Mary Geofrey
Dar es Salaam
Nipashe
Adha mwendokasi sasa kuwa historia

HATIMAYE changamoto ya usafiri katika Jiji la Dar es Salaam imepatiwa suluhu baada ya kujitokeza kwa mwekezaji mwingine katika mradi wa mabasi yaendayo haraka, maarufu mwendokasi.

Mwekezaji mpya huyo anatarajiwa kuongeza idadi ya mabasi yanayotumika katika mradi huo kutoka 140 ya sasa hadi 305, ambayo ndiyo makubaliano ya waendeshaji wa mradi huo na serikali.

Vilevile, waendeshaji wa mradi huo wamedai kutekeleza mapendekezo yaliyotolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuhusu mradi huo ulioanza mwaka 2016.Meneja Uhusiano wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart), William Katambi, aliweka wazi taarifa za neema hiyo alipozungumza na Nipashe jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.

Katambi alisema dawa ya kero na usumbufu mkubwa wanaopata watumiaji wa mabasi hayo itapatikana Machi mwakani.

"Serikali ipo katika hatua za kumpata mtoa huduma mwingine ambaye ataongeza idadi ya mabasi na kufikia lengo la kuwa na mabasi 305," Katambi alisema na kueleza zaidi:

"Tunatarajia mtoa huduma huyu mpya atakuwa ameanza kutoa huduma ifikapo Machi, 2019 na sasa watakuwa wawili na tunaamini hakutakuwa na matatizo tena.

"Mabasi kwa sasa ni machache kwa sababu serikali ilikuwa ikisubiri kumpata mtoa huduma atakayeendana na ushindani wa kimataifa kwa ajili ya kutoa huduma.

"Hiki ni kipindi cha mpito, ndiyo sababu awamu ya kwanza mabasi 140 yanayotoa huduma. Tuliona miundombinu imekamilika hivyo ni vyema tukaanza kutoa huduma wakati tukimsubiria mtoa huduma anayekidhi vigezo vya kimataifa, lakini tulianza na majaribio ya mabasi 140 ili kubaini dosari."Hata hivyo, hakuwa tayari kumzungumzia kwa undani mwekezaji mpya wa mradi huo.

Alisema wamekaa na wenye Kampuni ya Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (Udart) kuzungumza changamoto zilizopo kwenye mradi huo na kubaini kuwa changamoto kubwa ni uhaba wa mabasi na idadi kubwa ya watumiaji.Alisema kutokana na hali hiyo makundi maalum kama walemavu, wazee, wajawazito na wagonjwa hawapewi nafasi za kukaa kwenye viti, hivyo kuzidisha usumbufu.

Aliongeza kuwa Oktoba 10, mwaka huu, baada ya abiria wa Kituo cha Kimara kufanya vurugu zilizosababishwa na mabasi kuchelewa kufika kituoni, walifanya kikao na kuweka mikakati ya kuzuia usumbufu huo.

Alisema miongoni mwa mikakati hiyo ni kuhakikisha mabasi ya Udart yanaanza kutoa huduma saa 10:30 alfajiri ili kuondoa usumbufu kwa abiria.

"Tulikubaliana mabasi yawe yanachukua abiria vituoni kuanzia saa 10:30 badala ya saa 11 alfajiri, lakini tunatambua kwamba muda huo kuna changamoto ya kutokuta abiria wengi vituoni," alisema Katambi.

Aliwataka watumiaji wa mabasi hayo kubadilisha utaratibu wa kutoka nyumbani ili kupunguza usumbufu wanaokutana nao kuanzia saa 12 asubuhi wakati ambao watu huwa wengi vituoni.

Katambi pia alizungumzia upimaji wa mabasi hayo uliofanyika wiki iliyopita eneo la Jangwani, akibainisha kuwa lengo ni kutaka kufahamu uzito halisi wa mabasi hayo yakiwa yamepakia abiria.

Alisema kwa kufanya hivyo, watakuwa na maandalizi mazuri ya ujenzi wa barabara nyingine za mwendokasi zitakazojengwa katika maeneo mengine ya Jiji la Dar es Salaam ikiwamo Barabara ya Mandela.

HOJA ZA CAG

Katambi pia alisema wamefanyia kazi hoja zilizoibuliwa na CAG kuhusu mradi huo huku akibainisha kuwa hesabu zao hukaguliwa kila baada ya miezi mitatu.

Katika ripoti yake ya mwaka 2015/16 iliyowasilishwa bungeni Aprili mwaka jana, CAG Prof. Mussa Assad, alifichua udhaifu katika mradi huo.

Katika ripoti hiyo CAG alisema ukaguzi alioufanya kwenye mradi huo, ulibaini Dart ana upungufu mwingi.

Alisema katika mkataba wa utoaji wa huduma ya usalama katika vituo vya Dart na Jangwani, alibaini kuwa Mei 5, 2016 Dart iliingia mkataba wa miezi 12 na M/S China Tanzania Security Company Ltd wa utoaji huduma ya ulinzi kwenye vituo vya Dart na Jangwani kwa jumla Sh. milioni 178.652.

Prof. Assad alisema kuwa katika mapitio ya taratibu za ununuzi, ilibainika matangazo na zabuni zilizotolewa hazikuwasilishwa PPRA, mkataba ulisainiwa baada ya tarehe ya kukamilisha mkataba kuisha kinyume cha kifungu 370(1) cha Kanuni ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2013 na pia nakala ya mkataba haikuwasilishwa kwa Mwanasheria Mkuu kwa ajili ya kupitia na kuhakikiwa (Vetting) kinyume cha kifungu 59(1) na (2) vya Kanuni ya Ununuzi ya Umma za mwaka 2013.

"Kutokana na mazingira hayo ni vigumu kuthibitisha kwamba taratibu sahihi za ununuzi zilifuatwa katika utoaji wa huduma za usalama, na iwapo matumizi ya Sh. milioni 178.652 yalikuwa matumizi sahihi ya fedha za umma," alisema Prof. Assad katika ripoti hiyo.

CAG alipendekeza kuwa menejimenti ya Dart ifuate sheria na kanuni dhidi ya usimamizi wa mikataba na kuweka mikakati ya jinsi ya kutatua upungufu unaojitokeza, hivyo wahakikishe wakala wa serikali na taasisi nyingine wanaimarisha mifumo ya ndani ili kuhakikisha upungufu haujitokezi kwa baadaye.

Pro. Assad pia alisema kuwa katika ukaguzi wake alibaini Dart ilinunua bidhaa na huduma za jumla ya Sh. milioni 332.653 nje ya mpango wa ununuzi kwa ajili ya kukodi sehemu ya ndani, nishati na mnara wa mawasiliano kwa Sh. milioni 154 na kutoa huduma ya usalama katika vituo vyake na Kituo Kikuu cha Jangwani kwa kiasi cha Sh. milioni 178.652.

Alisema ununuzi huo ni kinyume cha Kifungu 69(3) cha Kanuni za Ununuzi wa Umma za mwaka 2013 kinachotaka taasisi inayofanya ununuzi kufanya makisio sahihi ya mahitaji ya bidhaa, huduma na kazi.

Alisema kuwa jumla ya mapato ya Sh. milioni 90.499 yaliyoonyeshwa kwenye taarifa za fedha yaliyotokana na matangazo katika miundombinu ya Dart, hayakuwa na uthibitisho zikiwamo nyaraka za ununuzi wa zabuni, jambo ambalo ni kinyume cha Kifungu 55(1) cha Kanuni za Ununuzi wa Umma za mwaka 2013, hivyo ilishindikana kuthibitisha usahihi wa taratibu za ununuzi.

"Napendekeza kuwa wakala wa serikali wafuate taratibu za ununuzi na kuandaa mikataba kwa kila taasisi inayotumia miundombinu ya Dart kufanya matangazo," alieleza CAG katika ripoti hiyo.

Prof. Assad pia alisema ukaguzi wake ulibaini Sh. milioni 372.6 zilitakiwa kulipwa na meneja wa mfuko wa ISP kwenda Dart kama ada ya ISP kati ya Mei 16, 2016 na Juni 30, 2016, lakini hadi kufikia Juni 2016, kiasi cha Sh. milioni 85 kililipwa na kubaki kiasi cha Sh. milioni 287 ambazo hazijalipwa na ISP kupitia meneja wa mfuko DART.

Alisema jambo hilo ni kinyume cha makubaliano kati ya Dart na Udart ya Mei 31, 2016 ambapo meneja wa mfuko alitakiwa kufanya malipo ya kila siku ya Sh. milioni 8.1 kwa wakala kama ada ya upatikanaji wa huduma.

"Na ikiwa siyo siku ya kazi, malipo yafanyike siku ya kazi inayofuata. “Kutokulipa ada ya upatikanaji wa huduma kunaathiri ukwasi wa wakala, na hivyo kuchelewesha utekelezaji wa shughuli zilizopangwa," Prof. Assad alisema.

Utoaji wa huduma ya mabasi hayo ulianza rasmi Mei 10, 2016 ikitolewa katika njia nane, vituo vikuu vitano, vituo vidogo 28 na karakana moja kwa kutumia mabasi 140 yanayojumuisha mabasi makubwa 39 yenye uwezo wa kubeba abiria 160 kila moja na mabasi madogo 101 yenye uwezo wa kubeba abiria 60 kila moja.

Habari Kubwa