Adha inayowakumba wasafiri kituo Mbezi Luis

02Mar 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Adha inayowakumba wasafiri kituo Mbezi Luis

KUKOSEKANA kwa utaratibu na mpangilio wa wafanyabiashara wadogo katika kituo kikuu cha mabasi cha Magufuli, Mbezi Luis, mkoani Dar es Salaam, kumesababisha kero kwa abiria, magari na kupoteza mwonekano mzuri wa kituo hicho.

Mamalishe wakiendelea na kazi zao katika eneo la kituo cha Magufuli Mbezi Luis Manispaa ya Ubungo, Dar es Salaam jana, wakisubiri kupangiwa eneo maalum la kufanyia biashara yao. PICHA: MIRAJI MSALA

Baadhi ya mamalishe wameonekana wakifanya biashara ya kuuza chakula huku wakiwa na majiko yenye moto, hali inayohatarisha usalama wa abiria na magari.

Mwandishi wa gazeti alishuhudia majira ya asubuhi wafanyabiashara hao wakiwa wamezagaa kila eneo bila kuwa na utaratibu mzuri wa mabasi kuingia kituoni hapo.

Utaratibu uliopo sasa mabasi yanakoingilia ndiko kwenye maegesho ya bajaj, pikipiki na magari binafsi, jambo linalosababisha adha kubwa kwa abiria.

“Kituo hiki ni kizuri sana cha kimataifa, lakini kukosekana kwa utaratibu maalum wa kufanya biashara humu kunakichafua na kuonekana cha ovyo, ona wafanyabiashara wako kila mahali na wengine wana majiko ya kupikia hii ni hatari sana,” alisema mmoja wa abiria, Monica John.

“Ona mama na baba ntilie wanauza chakula kila mahali, wengine wana majiko ya mkaa na kuni, na anakaa pembeni ya magari, inapoteza mwonekano, kama wanataka watu hawa wawepo kituoni ni muhimu kuwe na utaratibu mzuri ili kuwa na mwonekano mzuri na usalama,” alisema.

Kadhalika, kwa sasa magari yanayotoka mikoa ya Kusini yanapoingia Dar es Salaam, hayaruhusiwi kushusha abiria njiani mpaka kituo cha Mbagala na Temeke na kituo cha mwisho ni cha Mbezi.

Akizungumza na Nipashe kondakta wa moja ya gari linalofanya safari zake Kusini mwa Tanzania, alisema “Haturuhusiwi kushusha abiria zaidi ya vituo viwili yaani Temeke na Ubungo (kwa sasa Mbezi Mwisho), tukishusha njiani tunakamatwa.”
Mmoja wa abiria aliyekuwa ndani ya gari hilo aliyekuwa anashukia kituo cha Tabata Matumbi, Rosemary Joseph, alisema kumpeleka Mbezi mtu anayeshuka Tabata ni kumpotezea muda na kumsababishia gharama.

Abiria hao walishauri ni vyema serikali ikaweka utaratibu wa mabasi ya mikoa ya Kusini ambayo hupita Barabara ya Kilwa na yanayopita Barabara ya Bagamoyo kushusha abiria njiani, badala ya mpaka kupelekwa Mbezi.

Aidha, watumiaji wa kituo hicho waliomba uwekwe utaratibu maalum wa kuingia na kutoka kituoni humo ili kuondoa kero ya foleni katika makutano ya barabara hiyo ambayo kwa sasa hakuna taa.

“Kwenye makutano ya barabara ya Morogoro magari yanayotoka Ubungo yanayoelekea kituoni yanatakiwa kuzunguka kando kidogo ya barabara kuu na kuingia upande wa pili, huku yanayotoka Chalinze yanatakiwa kuzunguka ndiyo yaingie kituoni humo, bila kuweka utaratibu eneo hili limegeuka kuwa kero kubwa nyakati za asubuhi na jioni,” alisema mmoja wa abiria.

Akizungumza na Nipashe, Meneja wa Kituo cha Mabasi cha Magufuli, Maira Chilosa, alisema jana imefanyika operesheni ya kuondoa mamalishe waliokuwa na majiko ndani ya kituo na kuweka eneo maalum wakati wanasubiri ujenzi wa eneo la kupikia.

“Eneo lao (mamalishe na babalishe) limefanyiwa upembuzi yakinifu na baada ya kukamilika watakuwa na eneo la kupikia, kwa sasa tumewaondoa ndani ya kituo kwa kuwa ni hatari kwa magari na watu, anaruhusiwa kuuza vitu vilivyopikwa, vikavu na bidhaa nyingine na siyo kupikia ndani ya kituo,” alifafanua.

Alisema kituo hicho kinasimamia utekelezaji wa agizo la Rais John Magufuli kuwa wafanyabiashara wadogo waruhusiwe na kwamba utaratibu unafanyika ili kutowasumbua, lakini kuwe na utaratibu wa kutunza kituo hicho.

Kuhusu waendesha bodaboda na pikipiki, alisema wamepokea malalamiko ya kuongezeka kwa madereva wa vyombo hivyo huku wenyeji waliowakuta wakishindwa kufanyabiashara na kwamba jitihada za kuwaandalia eneo maalum unaendelea.

Kuhusu wapigadebe, alisema watu 48 wamekamatwa jana na kupandishwa mahakamani kwa kosa la kubugudhi abiria na kupigwa marufuku kupiga debe ndani na nje ya kituo hicho.

Akizungumzia mabasi yanayofanya safari mikoani, alisema magari yote yanatakiwa kuanzia ndani ya kituoni hicho na waliofungua ofisi za kupakia na kushusha abiria maeneo ya Shekilango hawaruhusiwi kufanya hivyo na watakaokaidi watachukuliwa hatua.

Nipashe iliwatafuta wasemaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Ardhini (LATRA), ambao walisema wana vikao vingi huku Mkurugenzi wa Udhibiti wa Huduma za Barabara, Johansen Kahatano, simu yake ikiita bila kupokewa.

Habari Kubwa