Afa ajalini akimkimbia trafiki

26Jan 2017
Ibrahim Yassin
MBOZI
Nipashe
Afa ajalini akimkimbia trafiki

MFANYABIASHARA Frank Mwanja, amefariki dunia papo hapo baada ya gari alilokuwa akiliendesha kupinduka, wakati trafiki aliyemsimamisha eneo la njiapanda ya kwenda kiwanda cha kusindika kahawa, mji mdogo wa Mlowo mjini hapa.

Ajali hiyo iliyohusisha gari dogo lenye namba za usajili T 959 ARC, pia ilimjeruhi mwanamke ambaye jina lake halikufahamika mara moja.

Wakizungumza jana na gazeti hili, baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo, walidai kuwa chanzo cha ajali hiyo kuwa ni baada ya mfanyabiashara huyo kujaribu kumkimbia askari wa usalama barabarani.

Walidai kuwa baada ya mfanyabiashara huyo kusimamishwa, walishindwana kauli na askari huyo na ndipo alipoliondoa kwa kasi gari lake.

Hata hivyo, alisema baada ya kufika eneo hilo, gari lake lilipinduka na kufa papo hapo.

Kamanda wa Polisi mkoani Songwe, Mathius Nyange, alisema baada ya ajali hiyo, polisi walikwenda eneo la tukio kuuchukua mwili wa marehemu na kuupeleka Hospitali ya Wilaya kwa uchunguzi na hifadhi huku mwanamke aliyejeruhiwa akipatiwa matibabu hospitalini hapo na hali yake inaendelea vizuri.

Kamanda Nyange alisema polisi wanaendelea kufanya uchunguzi zaidi wa tukio hilo.

Aidha, Kamanda Nyange amewataka madereva kuheshimu Sheria za Usalama Barabarani ili kuepusha vifo vinavyozuilika.

Habari Kubwa