Afariki kwa ajali ya moto nyumba yake ikiteketea

21Sep 2021
Cynthia Mwilolezi
Arusha
Nipashe
Afariki kwa ajali ya moto nyumba yake ikiteketea

MKAZI wa Mtaa wa Negamsi katika Mamlaka ya Mji wa Babati mkoani Manyara, Gift Mihayo, amepoteza maisha baada ya nyumba yake kuteketea kwa moto.

Inaelezwa kuwa Mihayo, kabla ya kufariki dunia, kutokana na majeraha ya moto huo, alikuwa akiendelea kuvuta sigara ndani, wakati nyumba ikiteketea kwa moto.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Kamishna Msaidizi, Marrison Mwakyoma, inadaiwa kuwa marehemu licha ya kuvuta sigara wakati nyumba hiyo inateketea, pia alikuwa amelewa pombe.

“Bado tunaendelea na uchunguzi wa tukio hili, lakini huyu Mihayo alifariki juzi usiku, ndani ya nyumba hiyo kulikuwa na mke na mtoto wake, walifanikiwa kutoka nje na kunusurika. Kuna taarifa kwamba wakati Mihayo akiwa ndani, mlango ulijifunga kabla hajatoka nje,”alisema.

Mwili wa Mihayo, umehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Babati ya Mrara ukisubiri taratibu nyingine za uchunguzi wa kitabibu.

Mmoja kati ya shuhuda wa tukio hilo, Abdi Kassim, alisema kuwa marehemu Mihayo alikuwa ni mpangaji kwenye nyumba hiyo.

“Mke wake akafanikiwa kumtoa mtoto nje na wakati anamfuata mume wake ndani, kwa bahati mbaya moto ukawa mkubwa na mlango ukajifunga na kushindwa kumuokoa,” alisema Kasim.

Alisema pamoja na jitihada za majirani waliotoka nje usiku huo, baada ya mwanamke huyo kuanza kupiga yowe na kuomba msaada hawakufanikiwa kumuokoa.