AFF, SUA waandaa mwongozo wa mabadiliko ya tabia nchi kwenye misitu

07Dec 2021
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
AFF, SUA waandaa mwongozo wa mabadiliko ya tabia nchi kwenye misitu

JUKWAA la Misitu Afrika (AFF) kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Kilimo chaSokoine (SUA), wameandaa mwongozo maalum wa kufundisha kozi fupi za mabadiliko ya tabia nchi kwenye misitu.

Washiriki wa semina ya kuwajengea uwezo wa masuala ya mabadililo ya tabia nchi kwenye misitu wakijadiliana mambo mbalimbali.

Akizungumza juzi wakati wa ufunguzi wa mkutano wa wataalamu na wadau wa misitu wa nchi za Cameroon, Uganda, Kenya, Msumbiji, Tanzania, Zambia na Zimbabwe, Katibu Mtendaji wa Jukwaa hilo, Prof. Godwin Kowero, alisema mwongozo huo utahusisha maeneo manane muhimu. Aliyataja maeneo hayo kuwa ni mafunzo ya sayansi ya awali ya mabadiliko ya tabia nchi kwa wanataaluma, kiufundi, misitu ya Afrika, soko na biasharaya kaboni kwa wananchi na wataalam, mifano ya hali ya hewa na maendeleo, mijadala ya kimataifa na mchakato wa kusukuma mbele hoja za nchi duniani, pamoja na mbinu mbalimbali. “Mwongozo huu wa mafunzo umetafsiriwa pia kwa lugha ya kifaransa. Zaidi umejikita kwenye maeneo matatu ya kukabiliana na mawili ya kupunguza mabadiliko ya tabia nchi kwenye misitu, Tupo hatua ya mwisho ya kukamilisha mwongozo wa kupunguza mabadiliko ya tabia nchi kwenye misitu kwa ajili ya wanataaluma,”alisema Kwa mujibu wa Prof. Kowero, matarajio ni kuwa mwongozo huo utaleta mabadiliko ya namna elimu na mafunzo yanatolewa na vyuo vikuu vingi Afrika, vyuo vya kati na taasisi za ufundi kuhusu mabadiliko ya tabia nchi kwenye misitu. “Tunaamini mwongozo huu wa kozi fupi utakuwa ufunguo wa haraka kuwajengea uwezo makundi mbalimbali kwenye mabadiliko ya tabia nchi kwenye misitu kwa Mashirika yasiyo ya kiserikali, wataalam wa ugani wa misitu na wafanyakazi kwenye taasisi za elimu na utafiti ambao hawajapata uelewa wa jambo hili,”alibainisha. Akiwasilisha mwongozo huo kwa washiriki wa mkutano huo, Ofisa Program Mwandamizi wa AFF, Prof. Marie Louise Avana, alisema kila somo litakuwa na matokeo maalum ya namna ya kutunza misitu na kupunguza mabadiliko ya tabia nchi kwenye misitu ambayo ni muhimu kwa maisha ya watu, viumbe na maendeleo. Mathalani, alisema katika mafunzo ya biashara na masoko ya kaboni, watakuwa na uelewa na kuweza kuchambua mbinu, uhusiano wake na kuuza mazao ya misitu, kutambua rushwa na mambo yaliyokinyume cha sheria kwenye biashara hiyo. Kwa mujibu wa Prof. Avana, mwongozo huo utasamabzwa kwa nchi zote zinazozungumza kiingereza na kifaransa na kwamba lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo washiriki wanaofanyakazi na jamii waiwezesha jamii kutambua fursa zilizopo kwenye misitu,sera, mipango na shughuli mbalimbali.

Habari Kubwa