AFP kushiriki marudio uchaguzi Z'bar

14Feb 2016
Mwinyi Sadallah
ZANZIBAR
Nipashe Jumapili
AFP kushiriki marudio uchaguzi Z'bar

HATIMAYE Chama cha Aliiance for Farmers Tanzanka (AFP) kimetangaza rasmi kuwa kitashiriki uchaguzi mkuu wa marudio utakaofanyika Machi 20, huku kikimtaka Amiri Jeshi Mkuu wa vyombo vya ulinzi, Rais John Magufuli kuimarisha ulinzi kabla na baada ya kufanyika uchaguzi huo.

Mgombea wa urais wa AFP Soud Said Soud

Kimesema wakati huu Zanzibar ikielekea katika maandalizi ya marudio ya uchaguzi yapo baadhi ya makundi na watu ambao wameanza kutoa matamshi ya vitisho dhidi ya raia, hivyo jukumu la kuhakikisha usalama na utulivu unadumishwa liko mikononi mwa Rais Magufuli.

Msimamo huo umetangazwa jana na mgombea wa urais wa ADP Soud Said Soud alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari huko Vuga Mkoa wa Mjini Magharibi kisiwani Unguja, akiwa na viongozi wa kitaifa wa chama hicho, katibu wake Shaibu Masoud Salum na mwenezi Abdalla Hassan Abdallah.

Alisema chama hicho kimetoa msimamo na kuamua kuingia katika uchaguzi baada ya kujiridhisha kuwa uchaguzi wa Oktoba 25 ulifutwa kisheri baada ya kujitokeza vitendo vya hila na udanganyifu kinyume na matakwa ya sheria na kuvunja misingi ya Demokrasia.

Soud ambaye pia ni mwenyekiti wa Taifa wa AFP alivitaja vitendo vya udanganyifu vilivyofanyika katika uchaguzi wa Oktoba 25 mwaka jana kuwa ni pamoja na watu kukamatwa na karatasi za kura katika mifuko ya suruali, kughushi maandishi ya matokeo ya kura, kufutwa namba za orodha ya wapiga kura na kuweka bandia huku mawakala wa vyama kupigwa na kufukuzwa katika vituo vya uchaguzi Pemba.

“Chama cha AFP kinatangaza rasmi kitashiriki uchaguzi mkuu wa marudio Zanzibar ili wananchi wapate fursa na haki ya kuchagua viongozi wao kwa njia za kidemokrasia na kutimiza matakwa ya katiba ya Zanzibar .”alisema.

Alisema kuwa wameamua kuingia katika uchaguzi huo baada ya kujiridhisha kuwa makosa mengi yaliyojitokeza katika uchaguzi wa Oktoba 25 mwaka jana yalifanywa kwa makusudi kwa kushirikiana na baadhi ya maafisa wa chama kimoja cha upinzani Zanzibar na sio viongozi wa Tume hiyo.

Alisema watendaji wa ZEC ndio waliohesabu kura nje ya vituo kinyume na sheria na taratibu na hatua ya ZEC kuwaondoa katika uchaguzi wa marudio ni uamuzi muafaka.

Akizungumzia kuhusu makamishina wawili wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) toka CUF na kutangaza kuwa hawakubaliani na kurudiwa kwa uchaguzi huo, alisema viongozi hao wamevunja kifungu cha 119 (10) kuwa maamuzi ya wajumbe wengi ndiyo uwamuzi wa Tume.

Alisema kuwa makamishina hao wanapaswa kuchukuliwa hatua za kisheria kutokana na kitendo chao cha kupinga maamuzi halali yaliyofikiwa na ZEC ya kurudiwa uchaguzi huo.

Alisema jambo la kushangaza uchaguzi mkuu umefutwa Oktoba 28 mwaka jana huku makamishina hao wamejitokeza kupinga maamuzi ya Tume Februari 7 mwaka huu baada ya kushiriki vikao mbali mbali huku wakipokea posho na mishahra ya taasisi hiyo.

Alisema kinachoonekana kwa makamishina hao walikuwa wakifanya kazi ya kutetea maslahi ya chama chao cha CUF badala ya kutekeleza majukumu ya Tume hiyo na huenda walikuwa wakisubiri maelekezo toka mahali fulani.

"Mbali ya kuvunja Katiba, pia wamekiuka kiapo cha kulinda siri za Tume katika utekelezaji wa majukumu yao, kama wangekuwa na ujasiri usio na shaka wangejiuzulu mapema iwapo hawakubaliani na maamuzi yaliyofanywa na Tume". alisema soud.

Makamishina waliojitokeza na kupinga hawakubaliani na kurudiwa uchaguzi mkuu ni Ayoub Bakar Hamad, (CUF) Nassor Khamis Mohamed (CUF) kati ya Wajumbe saba wa Tume hiyo ambapo katika kikao cha makamishna kura tano ziliafiki kurudiwa uchaguzi.

Hadi sasa vyama vilivyothibitisha ushiriki uchaguzi huo wa marudio ni Adc, Sau, Tadea, AFP na CCM.

Habari Kubwa