Afrika, Asia zatakiwa kusimamia maslahi yao

22Oct 2019
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe
Afrika, Asia zatakiwa kusimamia maslahi yao

MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan, amezitaka nchi wanachama wa Shirika la Mashauriano ya Kisheria za Asia na Afrika (AALCO) kusimama pamoja ili kutetea maslahi ya nchi zinazoendelea kupitia taasisi imara za kisheria pamoja na sheria za kimataifa.

Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, akifungua Mkutano wa siku tano wa 58 wa Mwaka wa Shirika la Mashauriano ya Kisheria kwa Nchi za Asia na Afrika (AALCO), katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam jana. PICHA: OMR

Samia aliyasema hayo jana kwa niaba ya Rais John Magufuli wakati akifungua mkutano huo wa 58 wa mwaka ambao unafanyika Tanzania kwa mara ya tatu.

Akizungumza katika mkutano huo ambao umewakutanisha zaidi ya wanachama 40, Samia alisema wanashuhudia vita vya wenyewe kwa wenyewe katika nchi zinazoendelea zikichochewa na nchi zilizoendelea ili kujipatia rasilimali za nchi husika.

"Ni jukumu letu kupitia taasisi zetu za kisheria kusimama kidete kulinda na kutetea maslahi ya nchi zetu," alisema Samia.

Alisema nchi zinatakiwa kupambana kuhakikisha zinakuwa na taasisi imara ambazo zimeanzishwa kwenye misingi ya usawa na kuheshimu utu ili kulinda maslahi ya mataifa.

"Tunapopambana kufikia malengo yetu, tunahitaji kusimama pamoja na kuimarisha umoja tulio nao kupitia mashauriano ya mara kwa mara," alisema.

Samia alizitaka nchi wanachama kuendelea kushirikiana ili kuendeleza na kuimarisha sheria za kimataifa zilizopo za mataifa ya Asia na Afrika.

Alisema ushirikiano utachangia pakubwa kwenye maendeleo ya sheria za kimataifa hasa katika maeneo yanayohusiana na biashara za kimataifa, uwekezaji, ulinzi na usalama kikanda.

Samia aliuambia mkutano huo kwamba Tanzania imekuwa na amani na majirani zake na ni kinara wa amani katika ukanda wa Maziwa Makuu na inachangia kwa kiasi kikubwa katika ukombozi wa kisiasa.

"Tumekuwa na imani madhubuti kwamba mahali ambako kuna utawala wa sheria kuna utengamano na sehemu ambako kuna utengamano kuna ustawi na maendeleo," alisema.

Alisema Tanzania inaendelea kulinda amani katika nchi za Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC), Sudan katika eneo la Darfur na Lebanon.

Samia alitumia fursa hiyo kuzitaka nchi zilizoiwekea vikwazo Zimbabwe, kuviondoa akisema nchi hiyo ni taifa huru ambalo linahaki ya kujiamulia mambo yake.

"Tunaamini nchi wanachama zitatoa sauti ya pamoja ya kukemea tabia ya baadhi ya mataifa kuingilia mambo ya ndani ya mataifa mengine ambayo yapo huru," alisema.

Habari Kubwa