Afungwa miaka 30 jela kubaka mtoto

14Sep 2020
Jumbe Ismaily
Singida
Nipashe
Afungwa miaka 30 jela kubaka mtoto

MKAZI wa Kijiji cha Bukatika Kata ya Matongo katika Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Shabani Salimu (25), amehukumiwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Singida kutumikia adhabu ya kifungo cha miaka 30 jela baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kumbaka binti mwenye umri wa miaka 13.

Katika shauri la jinai namba 135/2019 ilidaiwa na Mwanasheria wa Serikali, Elizabeth Barabara, kwamba mshtakiwa alitenda kosa hilo Juni 16, 2019 saa 9:00 mchana katika Kijiji cha Bukatika, Kata ya Matongo wilayani Ikungi.

Aidha, mwanasheria huyo alidai pia kwamba siku ya tukio binti huyo alikuwa ameenda kutafuta kuni na ndipo wakati akirejea nyumbani alikutana njiani na mshtakiwa, ambaye alimvuta na kumwingiza vichakani kisha kumbaka.

Kwa mujibu wa Barabara, wakati binti huyo alipokuwa akivutwa kupelekwa vichakani alijaribu kupiga kelele za kuomba msaada kwa wasamaria wema, lakini haikuwezekana kupata msaada, hali iliyomsaidia mshtakiwa huyo kumaliza matamanio yake.

Hata hivyo mwanasheria huyo alidai kuwa katika maelezo aliyotoa mshtakiwa kituo cha polisi alikiri kwamba alimtendea unyama binti huyo na alipofikishwa mahakamani alikana.

Hata hivyo, baada ya Salimu kukataa kutenda kosa hilo ndipo upande wa mashtaka ulipeleka mahakamani mashahidi kumi, walitoa ushahidi ambao haukutia shaka yoyote kuwa mshtakiwa ndiye aliyembaka binti huyo na ndipo mahakama ilipomtia hatiani.

Kabla ya kutoa hukumu kwa mshtakiwa huyo, Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Mkoa wa Singida, Robert Oguda, alisema vitendo vya ubakaji katika jamii vimezidi kushika kasi.

Hakimu Oguda alisisitiza kuwa ili liwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama ya mshtakiwa huyo, mahakama hiyo ina muhukumu mshtakiwa adhabu ya kutumikia kifungo cha miaka 30 jela.

Habari Kubwa