Afungwa miaka mitano kwa kuvunja, kuiba mali za shule

23Nov 2020
Samson Chacha
Tarime
Nipashe Jumapili
Afungwa miaka mitano kwa kuvunja, kuiba mali za shule

MKAZI wa Mtaa wa Serengeti, Tarime mkoani Mara, Francis  Mokera, amehukumiwa kifungo cha miaka mitano jela baada ya kupatikana na hatia ya kuvunja na kuiba mali za shule.

Mokera alihukumiwa juzi katika Mahakama ya Wilaya ya Tarime baada ya kukutwa na hatia ya kufanya kosa hilo na kuiba magodoro, viti na taa za umeme, mali za Shule ya Sekondari Tarime zenye thamani ya Sh. 2,850,000.

Akisoma Hukumu hiyo, Hakimu Mkazi Vincensia Balyahula, alisema ameridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka bila kuacha shaka.

Awali, Mwendesha  Mashitaka Thabiti Temba alidai mahakamani hapo kuwa mtuhumiwa alitenda kosa hilo baada ya kuvunja milango ya shule na kuiba vitu hivyo kati ya Machi na Mei, mwaka huu, hivyo kusababisha hasara kwa shule hiyo na wanafunzi kuathirika katika
masomo yao.

Hakimu Balyahula alisema: “Vitendo hivyo ni hujuma kubwa kwa wanafunzi, hivyo mahakama hii inakuhukumu kwenda kutumikia kifungo cha miaka mitano jela ili iwe fundisho kwa watu wengine wanaohujumu mali za umma na kuwarudisha wanafunzi nyuma kielimu."

Baada ya hukumu hiyo, walimu wa shule hiyo  waliokuwa nje ya mahakama, walisikika wakisema haki imetendeka.

Habari Kubwa