Agape watoa elimu ya ukatili, corona Mwamala

23May 2020
Marco Maduhu
SHINYANGA
Nipashe
Agape watoa elimu ya ukatili, corona Mwamala

Shirika la Agape ambalo linatetea haki za watoto  mkoani Shinyanga, limetoa elimu ya ukatili na jinsi ya kujikinga na maambukizo ya virusi vya corona kwa wajumbe wa kamati ya Mtakuwwa Kata ya Mwamala Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga.

Mkurugenzi wa shirika la Agape John Myola, wa kwanza kulia akitoa maelezo wakati akikabidhi vifaa vya kisasa vya kunawa mikono kwa sabuni na majitiririka ili kujikinga na maambukizi ya virusi vya Corona kwa wajumbe wa Mtakuwwa, Mwamala.

Elimu hiyo imetolewa jana Mei 22, 2020 katika ofisi ya Kata ya Mwamala kwa kukutana na wajumbe wa mpango mkakati wa Serikali wa kutokomeza ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto (Mtakuwwa) Kata hiyo.

Akizungumza wakati wa utoaji wa elimu hiyo Mkurugenzi wa Shirika hilo,  John Myola, amesema katika kipindi hiki cha janga la maambukizo ya virusi vya corona, wameamua kutoa elimu ya kujikinga na maambukizo hayo sambamba na ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto.

Amesema kuwa Shirika hilo kwa kushirikiana na wataalamu wa afya wanatoa elimu ya kujikinga na maambukizo ya corona katika maeneo ya vijijini pamoja na elimu ya kupinga ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto ili jamii ibaki kuwa salama.

Mkurugenzi wa Shirika la Agape, John Myola, akitoa elimu namna ya kunawa mikono kwa sabuni na majitiririka kabla ya kugawa vifaa hivyo Mwamala ili kujikinga na maambukizo ya virusi vya corona.
Afisa mradi wa kutokomeza ndoa za utotoni na ukatili dhidi ya wanawake na watoto, Sophia Rwazo, akiwataka wajumbe wa Mtakuwwa kutekeleza majukumu yao ili kufikia malengo ya kupunguza matukio ya ukatili ndani ya jamii

Mhudumu wa afya kutoka Samuye, Ilambona Alfred, akitoa elimu ya corona.

"Shirika letu la Agape tunaungana na Serikali kutoa elimu ya kujikinga na maambukizo ya virusi vya corona, pamoja na kupinga matukio ya ukatili katika maeneo ya vijijini na sasa tupo Kata ya Mwamala pamoja na kutoa vifaa vya kujikinga na maambukizi hayo zikiwamo ndoo za majitiririka na sabuni," amesema Myola.

Naye Afisa Maendeleo Kata ya Mwamala, Sophia Philbert, ambaye pia ni katibu wa Mtakuwwa, amewataka wajumbe hao kwenda kuwa mabalozi wazuri kwa wananchi katika kutoa elimu ya kujikinga na virusi vya corona, pamoja kuimarisha ulinzi dhidi ya watoto na kuwazuia kuzurura hovyo.

Kwa upande wake mhudumu wa afya katika kituo cha Samuye, Ilambona Alfred, ametoa elimu kwa wajumbe hao namna ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona, kunawa mikono mara kwa mara kwa sabuni na majitiririka, kukaa umbari wa mita moja, kuvaa barakoa, pamoja na kutokaa makundi.

Aidha Afisa Tarafa wa Samuye, Ntarle Magese, ametoa wito kwa wananchi kuacha kupuuzia janga hilo la maambukizi ya virusi vya corona licha ya kupungua, bali waendelee kuchukua tahadhari hadi pale Serikali itakapo tangaza janga hilo limeisha hapa nchini.

Habari Kubwa