Agizo la JPM kutengeneza ‘Ambulance’ latekelezwa siku 3

05Aug 2020
Julieth Mkireri
Pwani
Nipashe
Agizo la JPM kutengeneza ‘Ambulance’ latekelezwa siku 3

HATIMAYE Mkoa wa Pwani umetekeleza agizo la Rais Dk. John Magufuli la kufanyia matengenezo ya gari la kubebea wagonjwa katika Wilaya ya Rufiji.

Agizo hilo limetekelezwa zikiwa zimepita siku nne baada ya Rais Magufuli kuongea na wananchi wa wilaya hiyo Julai 30, akiwa njiani kutokea Mtwara na kuelezwa kuwa gari hilo ni bovu halitoi huduma kwa wagonjwa.

Rais Magufuli alitoa maelekezo kwa wilaya hiyo kutatua changamoto ya gari hilo haraka na kufanya kazi ya kuhudumia wagonjwa watakaohitaji huduma hiyo.

Akizungumza mjini Kibaha jana, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo, wakati akimkabidhi gari hilo Mganga Mkuu wa mkoa, Gunini Kamba, alisema wametekeleza agizo hilo Rais.

Mhandiai Ndikilo alisema gari hilo lilipelekwa kwa Wakala wa Huduma za Umeme na Ufundi (TEMESA) kwa ajili ya matengenezo na limekamilika tayari kwa kwenda kufanya kazi za kubeba wagonjwa.

“Tulitakiwa tutekeleze agizo ndani ya siku tano, lakini sisi siku moja kabla tumefanikiwa kukamilisha matengenezo na sasa namkabidhi Mganga Mkuu wa mkoa litapelekwa Rufiji," alisema Ndikilo.

Aliwataka waganga wakuu wa wilaya za mkoa huo kuhakikisha magari ya wagonjwa yanafanya kazi na kama kuna tatizo lirekebishwe mapema wasisubiri kukumbushwa wajibu wao na viongozi wakuu.

Alisema kuwa viongozi wote walio ndani ya mkoa watatue matatizo kabla viongozi wa ngazi za juu hawajafika na kuwakumbusha wakati yako ndani ya uwezo wao.

Katika hatua nyingine alisema kuwa tayari ujenzi wa vyoo saba na mabafu mawili unaendelea kwa ajili ya soko la Wilaya ya Kibiti na umefikia zaidi ya asilimia 65 hadi Jumamosi ni upauaji.

Alisema kuwa vyoo vyote saba na mabafu mawili vitakuwa vimekamilika kwa asilimia 100 Jumamosi Agosti 8, na kuanza kutumika kwa kuwa hatua ya kupaua na kuezeka itakuwa imekwisha na mifumo ya maji na umeme vitakuwa vimekamilika kwa muda huo.

Habari Kubwa