Agizo la JPM lamwibua DC

17Oct 2018
Na Mwandishi Wetu
HAI
Nipashe
Agizo la JPM lamwibua DC

SIKU moja baada ya Rais John Magufuli kuagiza wilaya zote zilizokutwa na dosari katika miradi wakati wa mbio za Mwenge wa Uhuru, kutoa maelezo ndani ya siku 10 na kurekebisha dosari hizo,-

Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya.

Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya, ameibuka na kusema mhandisi mwelekezi aliyejenga chini ya kiwango kichomeo cha taka katika Zahanati ya Kia, amerejesha Sh. milioni 8.6 zilizotumika kimagumashi.

Mradi huo uliokuwa umeelezwa kugharimu Sh. milioni 12, badala ya Sh. milioni tatu zinazotakiwa kutumika kwa mujibu wa BOQ (makadirio ya ujenzi), ulikataliwa kuzinduliwa na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2018, Charles Kabeho, kutokana na kujengwa chini ya kiwango.

Akitoa taarifa jana kuhusu utekelezaji wa agizo la Rais Magufuli, Sabaya alikiri ni kweli kwamba ulifanyika ubadhirifu katika ujenzi wa Zahanati ya Kia ambayo ilipewa fedha za ujenzi huo na kampuni ya uendelezaji wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (Kadco).

“KADCO ilitoa Sh. milioni 99 na katika fedha hizo, zilitengwa Sh. milioni 12 kwa ajili ya ujenzi wa Incinerators (vichomea taka) na Taasisi ya K.I.D.T iliyopo chini ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro ilipewa zabuni ya ujenzi wake, lakini wakati wa ukaguzi tukagundua kwamba vichomea taka vimejengwa chini ya kiwango.

“Pamoja na mambo mengine, pia kamati ya ulinzi na usalama imebaini kwamba viwango vya malighafi ya ujenzi iliyotumika ni ndogo ukilinganisha na kilichoandikwa kwenye ripoti ya ujenzi wa mradi huo. Tulikuta kwa mfano kichomea taka kimoja kinachosemekana kimetengenezwa kwa Sh. milioni 1.6 wameandika wametumia bati 15, lakini tunaona bati tatu juu ya paa.”

Kutokana na udanganyifu huo, Sabaya alieleza kwamba kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo iliagiza ufanyike uchunguzi wa haraka, kwa kumtumia mhandisi mwingine wa kujitegemea kuchunguza uhalali wa matumizi ya fedha za mradi huo na akabaini kwenye vichomea taka vyote viwili ambayo K.I.D.T ilidai imevijenga kwa Sh. milioni 12, vimetumia milioni 3.4 pekee.

Mkuu huyo wa Wilaya alieleza zaidi kuwa uamuzi waliouchukua kwa haraka ni kumwita Meneja wa K.I.D.T na mhandisi wake na ikaamua kuwazuia na kutoa maelekezo kwa vyombo vya ulinzi na usalama viwazuie mhandisi mwelekezi na fundi aliyehusika na katika mahojiano, wamekiri upungufu huo.

Sabaya amesisitiza kutokana na kukiri udhaifu huo, K.I.D.T na timu yake ikaamriwa irejeshe fedha za umma. Taasisi hiyo imerejesha tayari Sh. milioni 8.6.

Aidha katika taarifa yake, Sabaya alisema ameagiza Mganga Mkuu wa Wilaya (DMO), aandike madhaifu hayo yaliyojitokeza na asisitize kwamba wamejisahihisha na maelezo hayo yaandikwe kwa uwazi na yasomeke katika taarifa ya kiongozi wa mbio za Mwenge.

Oktoba 15 mwaka huu, Rais Magufuli alipokutana na kufanya mazungumzo na wakimbiza Mwenge wa Uhuru mwaka 2018, Ikulu Dar es Salaam, pia aliagiza wakuu wa mikoa na wilaya katika halmashauri tano ambazo zimefanya udanganyifu kwa miradi iliyotembelewa na Mwenge mwaka jana kutoonekana mwaka huu, wajieleze kwa kina kabla ya kuchukuliwa hatua.

Habari Kubwa