Agizo la JPM lazua kizaazaa

06Jan 2019
Mary Geofrey
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Agizo la JPM lazua kizaazaa

WAFANYAKAZI wa sekta binafsi waliofukuzwa kazi kabla ya umri wa kustaafu, wamefurika ofisi za Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Sekta Binafsi na Isiyo Rasmi (NSSF), kudai fao la kujitoa.

Rais John Magufuli

Hali hiyo imetokea siku  chache baada ya Rais John Magufuli, kuagiza kurejeshwa kwa utaratibu wa zamani wa wastaafu serikalini kupewa mafao ya mkupuo ya asilimia 50 badala ya asilimia 25 yaliyopendekezwa katika kikokotoo kipya.

 

Wakizungumza na Nipashe jana katika maeneo mbalimbali ya ofisi za NSSF jijini Dar es Salaam, ambako watumishi hao walifurika kudai fao la kujitoa, wananchi hao walimuangukia Rais Magufuli asikie kilio chao ili nao walipwe stahiki zao badala ya kuendelea kuzungushwa.

 

Zaina Juma, ambaye alifika ofisi za NSSF Mkoa wa Ilala, aliiambia Nipashe kuwa anaiomba serikali isikie kilio chao ili wapatiwe stahiki zao badala ya kuendelea kuzungushwa kila siku.

 

“Tangu nimeachishwa kazi kwenye kampuni ya Jamana mwaka 2017, nimekuwa nikienda ofisi za NSSF Ilala na kujaza fomu ya fao la kujitoa lakini nazungushwa na matokeo yake wametuambia tena kuna utaratibu mpya badala ya mtu kujitoa anatakiwa kujiunga na mfumo wa kuchangia kwa hiari,” alisema.

 

Alimwomba Rais Magufuli kuingilia kati suala hilo kwa sababu wao ni watumishi ambao wameshafukuzwa kazi kwa sababu ya kampuni kushindwa kujiendesha, mikataba kumalizika na hawajapata kazi kwa muda mrefu.

 

“Rais atusaidie na sisi tupewe fedha zetu ili tuanzishe biashara zetu na tuendeshe maisha yetu badala ya kuendelea kutangatanga mitaani bila shughuli maalum,” alisema.

 

Naye Steven John ambaye alikuwa mfanyakazi wa Kampuni ya CSI iliyoko Kipawa,  Dar es Salaam, aliyeachishwa kazi mwaka 2016, alisema mbali na kucheleweshewa malipo yao, watumishi wa NSSF wamekuwa na kauli chafu zinazowafedhehesha.

“Pia tunakosa imani na NSSF kwa sababu inakuwaje hela zetu lakini wanatusumbua. Tunachofahamu Rais Magufuli aliagiza mfumo wa ulipaji wastaafu utumike wa zamani nafikiri pia wanapaswa kutulipa fedha zetu sisi tuliaochishwa kazi,” alisema John.

 

Pia alisema baada ya kuzungushwa wanavunjika moyo wa kuwajiriwa tena katika sekta binafsi lakini pia wanashindwa kuendesha maisha yao ilhali wana fedha walizojiwekea akiba kwenye mfuko huo.

 

Naye Kelvin Richard aliyekuwa mfanyakazi kwenye kiwanda ya Konyagi alisema tangu kufungwa kwa kiwanda hicho mwaka 2017 hana shughuli ya kufanya na tayari amerudi kwenye umasikini na amefuatilia michango yake NSSF lakini hajapewa jibu la maana.

 

“Tunamwomba Rais Magufuli atufikirie na sisi watumishi wa sekta binafsi kwa sababu hatujafikia umri wa kustaafu na tayari waajiri wametufukuza kazi, tupewe hela zetu tukafie mbele kama alivyosema Rais badala ya kuzungukazunguka kwenye ofisi za NSSF kila siku bila majibu,” alisema Richard.

 

Nipashe ilimtafuta Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, William Erio, ili kuzungumzia kadhia hiyo ambaye alisema hajapokea taarifa za malalamiko hayo.

 

Alisema kama watapokea malalamiko hayo watayafanyia kazi kwa mujibu wa sheria, kwa kuwatambua mtu mmoja mmoja na ofisi aliyokuwa akifanyia kazi na si kundi la wafanya kazi kama ambavyo wamedai kulalamika.

 

“Bado sijapokea taarifa za malalamiko hayo kama ambavyo umenieleza na ni kwa sababu wakurugenzi wameshaondoka kazini muda huu, isipokuwa naweza kuwa na majibu sahihi kuhusu malalamiko hayo siku ya Jumatatu,” alisema Erio.

 

Akizungumzia fao la kujitoa, Erio alisema wanafanyia kazi maagizo yote yaliyotolewa na Rais Magufuli na kwamba kwa  sasa wanaendelea na taratibu za utekelezaji.

 

“Kama ulisikia vizuri yale maagizo yote ya Rais Magufuli tunayafanyia kazi na tayari kikao cha Bodi ya NSSF kimeshakaa kujadili namna ya kutekeleza yale maagizo,” alisema Erio.

 

MAAGIZO YA JPM

Desemba 28, mwaka jana, Rais Magufuli alimaliza mjadala kuhusu kikokotoo cha  mafao kilichotokana na kanuni mpya ya Sheria ya Hifadhi ya Mifuko ya Jamii ya mwaka 2018, baada ya kuamuru utumike utaratibu wa zamani katika kipindi alichokiita cha mpito hadi mwaka 2023.

 

Uamuzi huo utawanufaisha watumishi wa umma huku wale wa sekta binafsi walio NSSF, wakiendelea kupata asilimia 25 kama ilivyokuwa awali.

 

Rais Magufuli aliagiza kurejeshwa kwa utaratibu wa zamani wa wastaafu serikalini wa kupewa mafao ya mkupuo ya asilimia 50 badala ya asilimia 25 iliyopendekezwa katika kanuni hizo mpya.

 

Alisema hatua hiyo haitarajiwi kuyumbisha mifuko hiyo kwa kuwa hadi mwaka 2023, wanachama 58,000 wa mifuko hiyo ndio watakaokuwa wamestaafu.

 

 

 

Habari Kubwa