Agizo la Meya stakabadhi za kieletroniki lapuuzwa

25Jan 2017
Salome Kitomari
Dar es Salaam
Nipashe
Agizo la Meya stakabadhi za kieletroniki lapuuzwa

LICHA ya Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita, kuiagiza kampuni ya kukusanya ushuru wa maegesho ya magari kutoa stakabadhi za kielektroniki, kampuni hiyo inaendelea kutoa stakabadhi za kawaida.

Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita.

Jana Nipashe ilishuhudia katika mtaa wa Sokoine Kanda ya Ilala saa 9:11 watumishi wa kampuni husika ikiendelea kutoa risiti za kawaida zenye mhuri wa kampuni ya uwakala ya Kaps Ltd.

Moja ya risiti ambayo Nipashe iliiona ikitolewa kwa aliyeegesha gari yenye namba 628135 yenye mhuri wa kampuni hiyo.

Hata hivyo, mhusika alipotaka stakabadhi ya kielektroniki, mtoa stakabadhi huyo alidai:

“Mashine zimeharibika zinatoa risiti nyingi kwa wakati mmoja, hivyo tumeambiwa tutoe hizi za kawaida.”

Stakabadhi hiyo ilitolewa hatua chache kutoka zilipo ofisi za Meya huyo eneo la Karimjee.

Nipashe ilitembelea mitaa mbalimbali ya Jiji na kukuta watoza ushuru wakitoa stakabadhi za kawaida kwa madai kuwa ndiyo maelekezo waliyopewa na kampuni yao.

Hilo linakwenda kinyume na agizo la Meya Mwita, alilotoa mwishoni mwa mwaka jana kuwa matumizi ya risiti zisizo za kielektroniki zinazotolewa na mawakala wa utozaji ushuru wa maegesho ya magari, zitakoma kwa kuwa zinakwamisha juhudi za ukusanyaji mapato.

Meya Mwita alisema madereva wanaoegesha magari yao wakipewa risiti hizo wazikatae na kudai za kielektroniki.

Alisema wamebaini kuwapo kwa baadhi ya watoza ushuru ambao wamekuwa wakiwapatia risiti madereva zisizo za kielektroniki.

“Hili ni agizo ambalo nalitoa na tumekwishatoa mara kwa mara kwamba risiti zisizo za kielektroniki, ni marufuku, madereva wanaoegesha magari na kupatiwa risiti hizo wasizikubali, hazitambuliki na fedha zako zitakuwa zimekwenda bure,” alisisitiza Meya Mwita.

Hata hivyo, baadhi ya watoza ushuru hao katia eneo la Mtaa wa Samora, Nipashe iliwabaini wakitumia tiketi za kielektroniki na wengine za kawaida na kuleta mkanganyiko.

Aidha, madereva waliojaribu kuzikataa risiti za kawaida, walijikuta katika mzozo mkali na wakusanyaji ushuru hao.

Habari Kubwa