Agizo mikoa, wilaya usimamizi mwongozo biashara ya mazao

25Jan 2021
Ibrahim Joseph
Dodoma
Nipashe
Agizo mikoa, wilaya usimamizi mwongozo biashara ya mazao

VIONGOZI wa mikoa na wilaya  wametakiwa kusimamia mwongozo wa biashara wa mazao yanayotumia mfumo wa stakabadhi ghalani kwa mwaka 2021, ili kusaidia mkulima kutoingia kwenye  mikono ya madalali wa mazao yao.

Mrajis wa Vyama vya Ushirika nchini, Dk. Benson Ndiege, alitoa maelekezo hayo jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mwongozo wa mfumo wa  mazao ya stakabadhi za ghalani wa mwaka 2021.

 “Ninawaomba viongozi wote katika ngazi za mikoa na wilaya ambapo mazao yanayotumia mfumo wa ununuzi wa stakabadhi ghalani kusimamia utekelezaji wa mwongozo huu ili kuwasaidia wakulima wetu,” alisema.

Aliyataja mazao mapya yaliyoingizwa kwenye mfumo wa stakabadhi ghalani ni choroko, soya, ufuta, mbaazi na dengu.

Alisema mazao hayo yameingizwa kwenye mwongozo huo ambao utawataka wananchi wote kutumia ushirika katika kuuza mazao hayo.

Alibainisha kuwa mwongozo huo unatoa maelekezo  kuwa mazao hayo yatakusanywa kwenye ghala za  vyama za ushirika na kusafirishwa kwenda  kwenye ghala kuu za minada ya kuuza mazao.

Kadhalika, alisema  katika kutekeleza azma hiyo ya Serikali, Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC) kwa kushirikiana na Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB)  na Soko la Bidhaa Tanzania (TMX) wameandaa mwongozo huo wa biashara wa 2021.

Dk Ndiege  alisema taarifa za mazao yaliyopokelewa ghala kuu zitatumwa soko la bidhaa na kuuzwa kwa minada kwa njia ya kieletroniki.

Aliongeza kuwa mfumo huo utawasaidia wakulima wadogo na wakubwa kuingia kwenye mfumo wa kujadili bei ya mazao kwa pamoja  na kuwa na uwazi katika soko kwa wanunuzi.

Aidha, aliwataka wanunuzi wa mazao kuanza kujisajili kwenye soko la bidhaa nchini ili kujulikana wakati wa kuingia kwenye minada ya kununua mazao ya stakabadhi ghalani.

Naye, Kaimu Mkurungenzi Mtendaji wa WRRB, Asangye  Bangu, aliwataka waendesha maghala kujisajili na kuzingatia vigezo vya uhifadhi wa mazao ghalani.

Bangu aliwataka wenye madeni kuhakikisha wanalipa madeni yao yote ili kukidhi vigezo vya kupata leseni mpya za uendeshaji wa maghala nchini.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa TMX , Godfrey Malekano, alisema lengo la Serikali kuandaa mwongozo huo na mfumo wa 2021, ni kupanua wigo wa soko ndani na nje ya nchi.

Habari Kubwa