Agizo wakuu wa  shule uandikishaji

17Jan 2018
Dege Masoli
Nipashe
Agizo wakuu wa  shule uandikishaji

MKUU wa Wilaya ya Tanga, Thobias Mwilapwa, amewaagiza wakuu wa shule na walimu wakuu kutomkataa mtoto yeyote kwa sababu zozote watakazopelekewa kwenye shule zao kwa kuanza darasa la kwanza ama kidato cha kwanza wilayani kwake licha ya changamoto zilizopo.

Alitoa agizo hilo kwenye kikao cha wadau wa elimu cha Mkoa wa Tanga, kilichofanyika katika  shule ya Tanga ufundi  Jijini hapa na kusisitiza matatizo yaliyopo yasitumike kama sababu ya kuwakataa watoto hao na yatapatiwa ufumbuzi wakiwa darasani.

“Mimi kama mkuu wa Wilaya nayatambua yote, kila shida kila kero na kila tatizo, lakini pamoja na hayo sitapendezewa kupata taarifa za watoto kukataliwa kwa sababu yoyote ile iwe madarasa au madawati ….Yaserikali yatafanywa na serikali na  ya wadau yatafanywa na wadau, lakini hata walimu watafanya ya kwao,” alisisitiza Mwilapwa.

Meya wa Jiji la Tanga, Mhina Mustapha, licha ya kuzipongeza shule zilizofanya vizuri mwaka jana kwenye mitihani ya taifa, lakini alielezea namna alivyojipanga kuhakikisha elimu inakuwa mkombozi na haki kwa watoto, wazazi na hata taifa kwa ujumla.

Hata hivyo,  Ofisa Elimu (msingi) Jiji la Tanga, Khalfan Shemahonge, alielezea changamoto za upungufu wa walimu, vyumba vya madarasa na madawati na kwamba licha ya kuwapo kwa mapungufu hayo,  jitihada za kukabiliana nazo zinaendelea ili kutoathiri elimu.

“Uchakavu wa majengo na upungufu wa vyumba vya madarasa, ukosefu wa chakula kwa watoto shuleni na madawati ni miongoni mwa mambo yanayozikabili shule nyingi za Jiji la Tanga, hivyo jitihada zinahitajika kuzipatia ufumbuzi,” alisema Shemahonge.

 Aidha, alieleza  namna waraka wa serikali wa kuhusu elimu unavyowakwaza kutokana na wazazi kutochangia mambo yanayohusu elimu kwa watoto wao kwa madai kuwa hilo ni jukumu la serikali, hivyo kukwamisha mipango na harakati za kuiboresha.

Pia alisema migogoro ya mipaka ya ardhi katika maeneo ya shule ni mingi na  umekosekana ufumbuzi kutokana na wananchi kutotoa ushirikiano kwa uongozi wa shule husika , hivyo kuifanya isimalizike kwa wakati.

Habari Kubwa