Ahueni makali mgawo maji yanukia

21Nov 2021
Na Waandishi Wetu
Kibaha
Nipashe Jumapili
Ahueni makali mgawo maji yanukia

AHUENI ya mgawo wa maji unaoyakabili baadhi ya maeneo katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani, inanukia baada ya kuwapo taarifa za kuongezeka kwa maji katika Mto Ruvu.

​​​​​​​Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, alisema jana kuwa  amepokea taarifa kutoka Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kuwa wamewasha mtambo wa kuzalisha maji wa Ruvu Chini baada ya maji kuongozeka Mto Ruvu.

Vilevile, Bodi ya Maji Bonde la Wami/Ruvu imethibitisha kuwa kina cha maji jana kiliongezeka kutoka mita 0.2 mpaka 0.61.

Kunenge alibainisha hayo  alipotembelea shamba la raia wa China aliyekamatwa na bonde hilo kwa kosa la kuvuta maji kutoka Mto Ruvu bila kibali.

Alisema agizo la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kwa Bodi ya Maji Bonde la Wami/Ruvu kufuatilia sehemu ambazo zimechepushwa maji na kuyaruhusu kuingia mtoni, limezaa matunda.

"Ninapenda kuwapongeza Bodi ya Maji Bonde la Wami Ruvu kwa kufanya doria ambayo imezaa matunda kwani nimepokea taarifa kutoka DAWASA kuwa maji yameongezeka mtoni na kupelekea kuwashwa mtambo wa kuzalisha maji wa Ruvu Chini na pia bodi imethibitisha maji kuongezeka kutoka mita 0.2 mpaka 0.61 kwa leo (jana) mchana," alisema.

Kunenge aliagiza kusitishwa shughuli za kilimo cha umwagiliaji kwa wakulima waliokuwa wanatumia maji ya Mto Ruvu.

Alisema ni marufuku kwa mtu yeyote kuendelea kutumia maji ya Mto Ruvu kwa shughuli za umwagiliaji na mifugo hadi pale serikali itakapotoa taarifa nyingine.

Kiongozi huyo aliyekuwa ameongozana na kamati ya ulizi na usalama ya mkoa, Wilaya ya Bagamoyo na Kibaha, alishuhudia baadhi ya wakulima wakiendelea na shughuli za kilimo.

"Wakulima wote wenye vibali vya kutumia maji kwenye Mto Ruvu wasitishe shughuli zao hadi pale yatakapotoka maelekezo mengine, wanaonywesha mifugo na kutumia mashine pia waache mara moja kwani kuendelea kufanya hivyo ni kuhatarisha maisha ya wananchi," aliagiza.

Aliwaonya wanaoiba maji nyakati za usiku na kufanya shughuli za umwagiliaji, akiwataka kuacha mara moja na wakikaidi hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

Kunenge aliwaagiza wakurugenzi kuwafuatilia watendaji ambao wanashindwa kuwajibika kwenye maeneo yao na kuwachukulia hatua za kinidhamu.

Alitoa agizo hilo baada ya kubaini uwapo wa wakulima wa umwagiliaji ambao baadhi yao hawajafuata sheria huku mamlaka zinazohusika zikiwa hazina taarifa sahihi za uwapo wao.

Imeandikwa na Frank Monyo na Julieth Mkireri

Habari Kubwa