Ahukumiwa jela miaka 15 kwa udhalilishaji kingono

26Mar 2020
Pendo Thomas
KIGOMA
Nipashe
Ahukumiwa jela miaka 15 kwa udhalilishaji kingono

Mahakama ya Wilaya ya Kigoma imemhukumu Mohamed Athumani (23) kwenda jela miaka 15, fidia ya shilingi 500,000 na viboko vitatu baada ya kukiri kufanya kosa la udhalilishaji wa kingono dhidi ya binti mwenye umri wa miaka 16 anayefanya kazi za ndani.

Mtuhumiwa Mohamed Athumani akiwa chini ya ulinzi wa askari katika mahakama ya wilaya ya kigoma.

Kesi ya udhalilishaji wa kingono namba 31 ya mwaka 2020 inayomkabili kijana huyo, imesikilizwa kwa mara ya kwanza katika Mahakama hiyo.

Akisoma maelezo ya awali wakili wa Serikali, Benedict Kivuma mbele ya hakimu mfawidhi wa mahakama hiyo Kenneth Mutembei amesema mshtakiwa  alitenda kosa hilo Januari 7, 2020 mwaka huu katika eneo la mji mwema .

Kivuma alisema maelezo ya aliyetendewa kosa ni kuwa mshtakiwa alikuwa akimtaka kimapenzi  kwa muda bila mafanikio na siku ya tukio  akiwa ameagizwa dukani alimvuta kwa nguvu na kumpeleka kwenye chumba cha mlinzi karibu na alipokuwa akipita kisha kumuingizia vidole sehemu za siri kinyume na kifungu 138 kifungu kidogo cha kwanza( a) na cha pili (a) cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 marejeo ya mwaka 2002.

Baada ya maelezo ya kosa hilo kusoma  hakimu akamuuliza mshtakiwa kama ni kweli alitenda kosa hilo ndipo akakiri mbele ya mahakama hiyo kuwa alitenda tukio hilo na kuomba kusamehewa.

"Nikweli nilitenda tukio hilo naomba kusamehewa kwa kuwa ni kosa langu la kwanza na pia ninategemewa na mke, watoto na wazazi wangu " Alisema

Baada ya utetezi huo Wakili wa Serikali, Benedict Kivuma akaiomba Mahakama hiyo kutoa adhabu kali ili iwe fundisho kwa wote wanao fanya vitendo vya udhalilishaji wa kingono.

 Hakimu Mutembei akasema adhabu ya kosa hilo ni miaka 15 hadi 20 ila kwa kuwa hajaisumbua mahakama hiyo kwa kukubali kosa baada ya kufikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza akamuhukumu miaka 15 jela ,fidia ya laki tano na viboko vitatu .

Habari Kubwa