Ahukumiwa kunyongwa hadi kufa kwa kumuua mkewe, kunyofoa viungo vyake

21Oct 2021
Grace Mwakalinga
Mbeya
Nipashe
Ahukumiwa kunyongwa hadi kufa kwa kumuua mkewe, kunyofoa viungo vyake

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi ya Mkoa wa Mbeya, imemhukumu kunyongwa hadi kufa Mateso Shantiwa, mkazi wa Kitusi wilayani Mbeya, baada ya kupatikana na hatia ya kumuua mke wake Zaina Mela na kunyofoa viungo mbalimbali ili apate utajiri.

Hakimu Mkazi Mfawidhi Mkoa wa Mbeya, Zawadi Laizer, mwenye mamlaka ya nyongeza kutoka Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mbeya kusikiliza mashauri ya mauaji, ndiye alitoa hukumu hiyo jana.

Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Laizer alisema amemhukumu mtuhumiwa kwenye shtaka hilo namba 18/2017 baada ya kuridhishwa na ushahidi wa upande wa Jamhuri bila kuacha shaka yoyote kuwa mshtakiwa alimuua mkewe.

Hakimu Laizer alisema mshtakiwa Shantiwa alikuwa akituhumiwa pamoja na wenzake wawili ambao hawakukamatwa ambao alishirikiana nao kumuua mke wake na kunyofoa viungo kadhaa vikiwamo masikio na matiti kisha kupelekwa kwa mganga aliyewaahidi kupitia vitu hivyo angewatengenezea utajiri wa kudumu.

Kwa mujibu wa ushahidi uliotolewa wakati wa usikilizwaji shauri hilo, mshtakiwa Shantiwa alishirikiana na wenzake wawili kutekeleza mauaji ya mkewe kwa kuondoa viungo ambavyo ni matiti yote mawili, macho, vipande vya masikio na sura ya marehemu ili kwenda kutengenezewa utajiri.

Hakimu Laizer alisema alizingatia maelekezo ya pande zote mbili na maoni ya wazee washauri wa mahakama, lakini zaidi, mahakama imeridhika mshtakiwa kuhusika moja kwa moja kumuua mke wake na watu alioshirikiana nao kwa tamaa ya kupata utajiri licha ya kwamba mshtakiwa alikuwa akikana kutenda kosa hilo.

Mshtakiwa alikuwa akiwakilishwa na Wakili Hilda Mbele na kabla ya hukumu, aliomba kupunguziwa adhabu lakini upande wa Jamhuri kupitia wakili aliyekuwapo mahakamani, Davice Msanga, ukaiomba mahakama kutoa adhabu stahiki ili iwe fundisho kwa wengine ambao wanakubali kudanganywa na waganga wa kienyeji.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, mshtakiwa Shantiwa (34), alidaiwa kutenda kosa hilo Aprili 22, 2017 akishirikiana na wenzake wawili, jambo ambalo ni kinyume cha kifungu namba 196 na 197 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu sura ya 16 kilichofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Habari Kubwa