Ahukumiwa kunyongwa hadi kufa kwa kuua mke na watoto

15Jul 2020
Neema Hussein
Katavi
Nipashe
Ahukumiwa kunyongwa hadi kufa kwa kuua mke na watoto

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Sumbawanga mkoani Rukwa, imemhukumu Yustine Robert (35) kunyongwa hadi kufa baada ya kupatikana na hatia ya kumuua mkewe na watoto.

Akisoma hukumu hiyo jana katika Mahakama ya Mhakimu Mkazi mkoani Katavi, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga, David Mrango, alisema mtuhumiwa alitenda kosa hilo kinyume cha kifungu cha 196 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2002.

Jaji Mrango alisema kwamba mtuhumiwa alitenda kosa hilo katika eneo la Majimoto Wilaya ya Mlele mkoani Katavi Aprili 5, 2013 kwa kuwatupa kwenye kisima cha maji mkewe na watoto wake wawili.

Ushahidi uliotolewa na mashahidi wa nne wa upande wa mashtaka ulionyesha kuwa mtuhumiwa alikuwa na ugomvi wa kifamilia siku moja kabla ya vifo vya wanafamilia wake.

Mrango alieleza kuwa mashahidi hao walisema kuwa mtuhumiwa alisikika akisema atafanya tendo la kihistoria ambalo halijawahi kutokea katika eneo hilo.

Jaji Mrango alisema ushahidi ambao umemtia hatiani Yustine Robert ni ushahidi wa kimazingira, ambao umetosha kuthibitisha shtaka aliloshtakiwa nalo mtuhumiwa.

Naye Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Lugano Mwasubila, aliishukuru mahakama kwa kutenda haki ikiwa na kuitaka jamii kutokujichukulia sheria mkononi bali kuiacha sheria kuchukua mkondo wake.

Habari Kubwa