Ahukumiwa kunyongwa mpaka kufa kumwua mkukuu kwa kipigo

09Nov 2019
Hellen Mwango
Dar es Salaam
Nipashe
Ahukumiwa kunyongwa mpaka kufa kumwua mkukuu kwa kipigo

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, imemhukumu Ester Lyimo (41), kunyongwa mpaka kufa baada ya kupatikana na hatia ya kumwua mjukuu wake Naomi John (7) kwa kipigo.

Lyimo ambaye wakati hukumu yake inasomwa kuanzia saa 8:18 mpaka saa 9:12, alisimama kizimbani macho makavu bila kuonyesha dalili za kusikitika wala kujutia tukio hilo.

Akisoma hukumu hiyo, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Pamela Mazengo, aliyesikiliza kesi hiyo katika mahakama hiyo iliyopewa mamlaka ya kusikiliza kesi za mauaji, alisema bila kuacha shaka mahakama yake inamtia hatiani.

"Kama kungekuwa na adhabu nyingine zaidi katika mauaji ningeitoa hiyo. Mahakama yangu inakuhukumu kunyongwa mpaka kufa kwa kumwua Naomi kwa makusudi," alisema Msajili.

Alisema mahakama yake imezingatia wakati ushahidi wa Jamhuri unatolewa mahakamani, mshtakiwa alipoonyeshwa kielelezo namba moja ambacho ni picha tisa zilizoonyesha mwili wa marehemu ukiwa na majeraha mbalimbali mwilini na damu mpya kuvilia kwenye ubongo, mshtakiwa alijibu picha hizo ni za kawaida.

"Mshtakiwa ulipoonyeshwa picha za mwili wa marehemu zilizojaa majeraha ikiwamo sehemu za siri, hukujali, hukuonyesha kujutia wala kusikitikia kitendo hicho wakati wewe ndiye ulikuwa na jukumu la kumlea lakini ulimsababishia majeraha ukamwacha bila kumpeleka hospitalini kupata matibabu mpaka akafa," alisema Msajili Mazengo.

Alisema ushahidi wa Jamhuri bila kuacha shaka umethibitisha kosa la mauaji na umeungwa mkono na maelezo yake ya onyo mshtakiwa aliyokiri kumpiga mtoto huyo mara kwa mara.

Mazengo alisema sababu za kifo hazina ubishi kwamba ni kipigo kutoka kwa mshtakiwa ambaye alikuwapo eneo la tukio na kwamba ni wazi alikuwa na nia ovu.

Mapema mahakamani hapo, Daktari Msaidizi Mwandamizi, Modesta Lasana (52), alidai kwamba uchunguzi wa kifo cha Naomi ulionyesha kwamba alikufa kutokana na mivunjiko mwilini ikiwamo fuvu la kichwa kupasuka, damu kuvilia kwenye ubongo na majeraha yaliyotoa usaha.

Akiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi Cecilia Mkonongo, shahidi alidai kuwa alikabidhiwa mwili wa Naomi aufanyie uchunguzi na kwamba kazi yake ina hatua mbili tofauti, ya kwanza nje ya mwili na pili ndani ya mwili.

"Nje ya mwili wa Naomi kulikuwa na makovu ya zamani na majeraha yaliyokuwa na vidonda vilivyotoa usaha ikiwamo sehemu zake za siri kuonyesha michubuko ya kitu kigumu,tumbo lilikuwa limesinyaa kwa kukosa chakula muda mrefu na makalio yalikuwa na vidonda vya kuunguzwa moto" alidai shahidi na kuongeza:

"Kwa upande wa ndani, kwa kuwa kichwa kilivimba nilifungua nikaona fuvu lilikuwa limekatika, damu mpya na ya zamani ilisambaa kwenye ubongo, mkono mmoja ulivunjika mara mbili na bega lilishuka."

Shahidi mwingine, Inspekta wa Polisi Salma Sechonge (43) alidai kuwa mshtakkwa alikiri kumpiga mjukuu wake Naomi John (7) (wakati wa uhai wake) mara kwa mara pamoja kumfinya sehemu mbalimbali za mwili wake.

Kadhalika alidai kuwa alipomhoji mshtakiwa alikiri kurudia kumpiga na kumfinya sehemu zenye majeraha katika mwili wa Naomi.
Shahidi mwingine, mtaalamu wa kupiga picha na kuchora ramani wa Jeshi la Polisi, Sajenti Mgeni (52), alidai kuwa alipewa kazi ya kupeleleza tukio la mauaji.

Alidai kuwa Machi 26, 2017 alipofika ofisini bosi wake alimkabidhi jalada la kupeleleza likiwa na watuhumiwa watatu wote wanawake, Ester Lyimo, Victoria John na Jacqueline.

Alidai kuwa kabla ya kuwahoji alimfahamisha bosi wake Mkuu wa Upelelezi wa Mbagala, Walelo, kwamba anataka kwenda eneo la tukio.

Shahidi huyo alidai kuwa aliongozana na askari wenzake Aloyce na mtoto wa mshtakiwa Victoria kwenda nyumbani kwake kwa sababu hawakupafahamu.

"Tulipofika tulipokelewa na watoto wawili wa kiume akiwamo Andrew ambaye alikuwa na mikwaruzo usoni, shingoni na mkononi nilianza kumhoji akanieleza majeraha hayo yametokana na kupigwa na mama mdogo. Nilipomfunua alikuwa anatisha zaidi ngozi ilikiwa ina majeraha kama kenge," alidai shahidi na kuongeza kuwa:

"Nilipomuona Andrew katika hali ile nikabaini kwamba walifanyiwa ukatili wa hali ya juu tofauti ni kwamba huyu mzima na yule amefariki, nilimpigia simu Afande Walelo akaniamuru nirudi kituoni na huyo mtoto."

Sechonge alidai kuwa alishuhudia jinsi Naomi (marehemu kwa sasa) alivyotumikishwa kazi za watu wakubwa tofauti na umri wake.

Alidai kuwa Mwanahamisi alijaribu kumsihi asiwapige lakini aliambua kununiwa, alipomsalimia hakuitikia na ikawa hawana mahusiano ya ujirani tena na kwamba alipomfikisha Andrew kituoni bosi wake alipomwona aliagiza apelekwe hospitalini na kwamba alilazwa.

"Machi 28, 2017niliungana na jopo la madaktari kufanya uchunguzi kwa kweli hali ya mwili wa marehemu ilisikitisha alikuwa na uvimbe mkubwa kichwani walipomfunua walibaini damu ilivilia kwenye ubongo, vidonda mwili mzima vilivyokosa matibabu na mkono wa kulia ulikuwa umevunjika" alidai shahidi huku akitokwa machozi ya uchungu.

Shahidi mwingine kutoka Dawati la Jinsia Polisi, Chang'ombe Koplo Joyce alidai kuwa siku ya tukio alipigiwa simu na Dk. Ruth anayehusika na ustawi wa jamii hospitali ya Temeke aende kuna tukio.

Alidai kuwa alikwenda kitengo cha dharula akafahamishwa kwamba wamepokea mtoto lakini mshtakiwa na wenzake wanadai ni mgonjwa wakati tayari ameshafariki dunia.

Andrew John (9) alidai mahakamani katika kesi ya mauaji ya Naomi John (7) kwamba alimwona mama yake wa ubatizo, Ester Lyimo akimpiga mpwa wake mpaka akafariki dunia .

Andrew ambaye alikuwa akiishi nyumbani kwa mshtakiwa kwa sasa anaishi Moshi mkoani Kilimanjaro, mbali na kumwita mama wa ubatizo ni mama yake mdogo.

Dk.Abdukarimu Hasan (36)kutoka Hospitali ya Rufaa Temeke alidai kuwa siku ya tukio mshtakiwa aliongozana na watoto wake wawili huku akiwa amembeba mgongoni mtoto na mwingine mdogo wa miezi saba akiwa amembeba mkononi.

Alidai kuwa anamfahamu mshtakiwa alikwenda ofisini kwake na alipofika kitengo cha dharula kati ya saa 6:00 na saa 7:00 mchana alionyesha kupaniki na hofu na kwamba alijitambulisha amempeleja mjukuu wake anasumbuliwa na malaria.

Katika kesi ya msingi, ilidaiwa kuwa Machi 25, 2017 Tuangoma Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam mshtakiwa alimwua mjukuu wake kwa kumpiga.

Habari Kubwa