Aidai hospitali bil. 1.5/- kwa madai kumsababishia utasa

27Sep 2021
Hellen Mwango
Dar es Salaam
Nipashe
Aidai hospitali bil. 1.5/- kwa madai kumsababishia utasa

FLORAH Lengwana, mkazi wa jijini Arusha, amefungua kesi ya madai Mahakama Kuu jijini Dar es Salaam dhidi ya Hospitali ya Kairuki na daktari wake, akidai fidia ya Sh. bilioni 1.5 kwa madai ya uzembe na uharibifu uliosababishwa wakati akipatiwa matibabu kati ya mwaka 2018 na 2019.

Katika kesi hiyo Lengwana anataka hospitali hiyo kumlipa fidia ya Sh. milioni 800 ya uharibifu uliosababishwa, Sh. milioni 80, malipo ya adhabu, Sh. milioni 700 uharibifu wa jumla na amri nyingine ni hospitali hiyo na daktari kwa uzembe na kumsababishia madhara.

Mlalamikaji, anaituhumu hospitali hiyo na daktari wake kwa pamoja kwa uzembe uliosababisha madhara makubwa yasiyorekebishika ya kuondolewa kizazi na kupoteza tena tumaini au nafasi yoyote ya kushika mimba au kuzaa watoto.

Kesi hiyo inatarajiwa kuanza kusikilizwa ushahidi wa mlalamikaji Oktoba 21, mwaka huu mbele ya Jaji Lilian Itemba.

Hatua hiyo imefikiwa baada ya pande zote mbili kushindwa kufikia makubaliano kwa njia ya usuluhishi.

Ilidaiwa katika hati ya madai kuwa Julai 2, 2018, wakati hakuwa mgonjwa au kusikia maumivu yoyote, mlalamikaji alikwenda hospitali kwa madhumuni ya kufanya uchunguzi wa saratani ya kizazi, ambayo hapo awali alikuwa akifanya kawaida kila baada ya miaka mitatu.

Alidai alipofika mapokezi ya hospitali hiyo na baada ya kusajiliwa, mlalamikaji alishauriwa kuwa kabla ya kufanyiwa uchunguzi huo lazima kwanza amuone daktari wa magonjwa ya wanawake, ambaye ilidaiwa alikuwa Dk. George Chugulu kwa kujaza fomu za NHIF ili aweze kuhudumiwa.

Pia, ilidaiwa mlalamikaji alimweleza Dk. Chugulu historia fupi ya kiafya ambayo naye aliagiza afanye vipimo vingine kadhaa, pamoja na Hysterosalpingography (HSG) na suala la uchunguzi wa saratani halikushughulikiwa.

Hati hiyo ya madai iliendelea kueleza badala yake, Dk. Chugulu anadaiwa alimshauri mlalamikaji huyo afanye vipimo vya utasa kabla ya kuruhusiwa kufanya uchunguzi wa Paps Mear.

Mlalamikaji alidai kupitia hati yake ya madai kuwa ushauri wa daktari na jinsi alivyoshughulikia suala lake ulijaa uzembe na usiokubalika.

Katika majibu yao, walalamikiwa wote kwa pamoja wamekanusha madai hayo katika hati yao ya pamoja ya utetezi na wanamtaka mlalamikaji huyo athibitishe madai hayo.

Pia kwa ufafanuzi Dk. Chugulu anapinga kuwa na uhusiano wowote na Hospitali ya Kairuki.

Walalamikiwa wanasema kuwa mlalamikaji alifika hospitalini Julai 2, 2018, akitaka ushauri wa daktari kuhusu malalamiko yake yanayohusiana na kutokuwa na ujauzito kwa zaidi ya miaka sita tangu amzae mtoto wake wa pekee aliyezaliwa baada ya kufanyiwa matibabu tofauti katika hospitali kadhaa.

Wanadai kuwa baada ya kuelezea maisha yake na historia ya matibabu, Daktari Chugulu alishauri kufanya vipimo alivyofanyiwa mlalamikaji, ambavyo vilikuwa muhimu kujua sababu ya shida zake na hatua inayowezekana ya kusaidia katika kutatua shida hiyo.

Walalamikiwa wanadai kuwa hakukuwa na uzembe au kitu chochote kibaya kwa ushauri uliopewa mlalamikaji, ambao aliukubali kwa yeye kusaini fomu za NHIF na kuonyesha utayari wa kufanyiwa vipimo vya matibabu katika maabara na Idara ya Radiolojia ya hospitali hiyo.

Habari Kubwa