Aishi kwa mateso baada ya kupooza, ndugu kumtelekeza

14Jan 2019
Elizaberth Zaya
Dar es Salaam
Nipashe
Aishi kwa mateso baada ya kupooza, ndugu kumtelekeza

NI miaka mitano sasa Emaculata Charles (37), mkazi wa Gongolamboto, Ilala jijini Dar es Salaam, anaishi kwa mateso baada ya kupooza na kutelekezwa na ndugu zake.

Ugonjwa huo ulianza taratibu mwaka 2002 kwa kupata ganzi miguuni na ilipofika mwaka 2014 alipooza kuanzia kiunoni hadi miguu na kumfanya aishi kwa upweke akitegemea msaada wa majirani na wasamaria wema.

Msaada mkubwa anaouhitaji kwa sasa ni kifaa maalum ambacho kitamwezesha kutembea na kufanya shughuli zake mwenyewe, kinachogharimu Sh. 2,550,000.

Akisimulia tatizo lake kwa mwandishi wa gazeti hili kwenye chumba alichofadhiliwa na msamaria mwema, Emaculata alisema, hali ya maisha yake ni ya shida na amekuwa akishinda ndani tangu kipindi hicho huku kula na huduma nyingine akitegemea msaada wa wasamaria wema.

Msaada anaoupata kwa wasamaria wema tangu kipindi hicho ni mahali pa kuishi, chakula na huduma za kusafishwa mwili kutokana na kushindwa kujihudumia.

Emaculata alisema pamoja na kuwa na ndugu zake, lakini wamemtelekeza, hawamsaidii wala hawana mawasiliano naye.
Alisema tatizo hilo lilimuanza tangu mwaka 2002 baada ya kuhitimu kidato cha nne.

Alisema mwanzoni alianza kusikia ganzi kwenye miguu yake, wakati huo akiwa anaishi na dada yake na baada ya kufika katika kituo cha afya alishauriwa akafanye uchunguzi zaidi.

Hata hivyo, alisema hakuwa na pesa ya kwenda kufanyiwa uchunguzi hivyo aliendelea kuishi kwa kutumia dawa za kupunguza maumivu.

Licha ya kuwa na tatizo hilo, alijiunga na mafunzo ya uuguzi mwaka 2005, wakati huo hali ya ganzi ilikuwa ikibadilika badilika kwa kupungua na kuongezeka.

Imaculata anasimulia kuwa aliwaeleza ndugu zake hali hiyo, lakini hawakuchukulia uzito, hivyo aliendelea kusoma huku tatizo hilo likimsumbua.

Alisema mwaka huo huo wa 2005 tatizo lilizidi kuongezeka, lakini hakukata tamaa akawa anaendelea kutumia dawa za kutuliza maumivu.

Mwaka 2006 akiwa mwaka wa pili, alipata ugonjwa wa kiharusi, lakini Mungu alimsaidia akapata nafuu baada ya kufanyiwa mazoezi na akaweza kutembea kwa msaada wa magongo.

“Kadiri siku zilivyozidi kusonga mbele tatizo lilizidi kuwa kubwa, nilikuwa naishi na dada yangu, akaondoka na hakurudi tena kwa hiyo ikawa ni kama amenikimbia,” alisimulia Emaculata na kuongeza:

“Dada mmoja alikuwa jirani yetu akanichukua na kunipeleka kunitibia kienyeji, kumbe ndio ilikuwa kama ananiongezea tatizo. Ilibidi niwaambie ndugu zangu ambao walikuwa wanaishi mkoani, wakasema watakuja, lakini hawakuja.”

Alisema, aliendelea kuishi hivyo huku akitembea kwa shida kwa msaada wa magongo kwenda shule, lakini wakati anamalizia masomo ya uuguzi mwaka wa tatu 2007, hali ilizidi kuwa mbaya na mahudhurio yake yakawa mabovu chuoni.

“Maumivu yalivyozidi nilikuwa napata shida sana, ilikuwa inafika wakati nahudhuria shuleni hata mara mbili kwa mwezi, lakini nashukuru Mungu nilimaliza,” alisema Emaculata.

Alisema mwaka 2014, alipooza kuanzia kiunoni hadi miguuni na hali ilizidi kuwa mbaya zaidi.

“Hapa ndipo hali ilizidi kuwa mbaya zaidi, hata yule dada aliyekuwa ananisaida alichoka, nikapiga simu kwa ndugu zangu kuwaeleza, lakini hakukuwa na msaada,” alisema Emaculata na kuongeza:

“Kuna dada niliyekuwa nasoma naye chuo, ndiye akaja kunichukua kuhangaika kufanya vipimo vya hapa na pale, nimefanya vipimo vingi mno na kuandikiwa dawa tofauti, dawa nyingine nilifanikiwa kuzinunua na nyingine sikufanikiwa na kwa sababu sikuwa na kazi hali ilikuwa ni ngumu sana kumudu mpaka nilipofikia katika hali hii.”

Alisema madaktari wamemwambia upo uwezekano mkubwa wa yeye kutembea tena endapo atapata kifaa maalum cha mazoezi.

“Wakati nimeenda kupima madaktari waliniambia kwamba kuna kifaa maalum ambacho nikikipata naweza kutembea na kinagharimu Sh. 2,550,000. Nawaomba Watanzania wenzangu wanisaidie. Nitashukuru sana hata kama akijitokeza mtu akaenda kununua na kuniletea. Natamani niweze kufanya shughuli zangu mwenyewe za kujipatia kipato, nimechoka na haya maisha,” alieleza Emaculata.

Aliomba kwa yeyote atakayeguswa awasiliane naye kwa simu namba 0719 464341.

Kutokana na maradhi hayo kuugua muda mrefu, Emaculata uwezo wake wa kusikia umeathirika, hawezi kusikia vizuri wala kuzungumza vizuri.

Alisema msaada mkubwa kwa sasa anaupata kutoka kwa mjumbe wa shina namba tisa, Kata ya Gongolamboto, Getnus Mienzi.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, mjumbe huyo alisema: “Nimemfahamu Emaculata tangu mwaka 2014 nilipopata taarifa za kuugua kwake na kwenda kumtembelea hapo anapoishi na nilipomuona alikuwa ni mtu mwenye uhitaji maalum, japokuwa niligundua kwamba alikuwa na ufahamu mkubwa sana. Kwa hiyo tangu kipindi hicho nikawa nimepata jukumu la kwenda kumwangalia mara kwa mara, kujua kama ana chakula au hana na kama nina chochote huwa namsaidia,” alisema Mienzi na kuongeza:

“Kiukweli sijawahi kuwaona ndugu zake, kwa ufupi Emaculata ni mtu ambaye ametelekezwa, kama unavyomuona yeye ni wa ndani, huduma yoyote anayohitaji ni mpaka ajitokeze wa kumsaidia, peke yake hawezi. Kama alivyojieleza mwenyewe anahitaji msaada wa hali na mali ikiwamo hicho kifaa cha mazoezi, tunaomba yeyote mwenye kuguswa aje amsaidie na wanaweza kufika anapoishi wajionee hali halisi,” alisema.

Habari Kubwa