Ajali Coaster, UDART zilivyoua Mwanza, Dar

20Apr 2019
Na Waandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Ajali Coaster, UDART zilivyoua Mwanza, Dar

AJALI mbili zilizotokea katika majiji ya Mwanza na Dar es Salaam zilizohusisha gari la Coaster na basi la Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka(Udart), yamesababisha vifo vya watu wanne.

Katika ajali ya kwanza, watu watatu wamefariki dunia na wengine 48 kujeruhiwa vibaya baada ya gari aina ya Coaster iliyokuwa inatoka Igombe wilayani Ilemela kwenda jijini Mwanza kupata ajali baada ya kupasuka tairi la mbele.

Tairi hilo ni la upande wa kulia kisha kutumbukia kwenye mtaro wa maji katikati ya daraja la Kona ya Malaika jirani na Uwanja wa Ndege wa Mwanza.

 

Ajali hiyo iliyotokea Alhamisi mchana,  wakati dereva wa gari hilo namba  T 454 AMQ alipojaribu kulipita lori la mchanga lililokuwa mbele kabla ya kugonga uzio wa daraja na kupasuka tairi na kutumbukia katika mtaro.

 

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa Sekou Toure, Dk. Bahati Msaki, alisema walipokea majeruhi 48 na maiti mbili, ambapo 16 walitibiwa na kuruhusiwa.

Alieleza kuwa 18 hali zao zilikuwa mbaya, hivyo kuwahamishia katika Hospitali ya Rufani ya Kanda Bugando na wengine saba kubaki Sekou Toure.

Daktari Bingwa wa magonjwa ya dharura na ajali, ambaye pia ni Kaimu Mkuu wa Idara ya Dharura katika Hospitali ya Bugando, Dk. Erasto Sylivanus, alisema majeruhi waliowapokea ni 18, ambapo wanaume ni 10, wanawake 8. Wamo pia watoto wawili na kati ya hao watano walifanyiwa upasuaji.

“Majeruhi watano ambao walikuwa wamepata majeraha katika maeneo ya ubongo, tumbo na mfupa tuliwafanyia operesheni, lakini kati ya hao majeruhi mmoja mwanamke ambaye hajatambulika alifariki dunia wakati akiwa katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) kutokana na kuumia katika maeneo ya tumbo, sehemu za ubongo na mifupa,” alisema Dk. Erasto.

Vilevile Erasto alisema, dereva wa gari hilo, Mwaka Isabuki yupo ICU kutokana na kuumia katika sehemu ya ubongo.

Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Dk. Philis Nyimbi, akizungumza baada ya kuwatembelea majeruhi waliolazwa katika Hospitali za Sekou Toure na Bugando, alisema wamiliki wa magari wanapaswa kuyafanyia matengenezo mara kwa mara na kuhakikisha madereva wanafuata sheria ili kuepusha ajali zinazoweza kuepukika.

Majeruhi waliohojiwa Ibrahimu Mtuly (Sekou Toure) na Dosele Mbute (Bugando) walisema, chanzo cha ajali ni tairi la upande wa kulia wa Coaster hiyo kupasuka, baada ya dereva kujaribu kulipita lori la mchanga.

Katika ajali ya pili, mtu mmoja anadaiwa kupoteza maisha kutokana na ajali iliyotokea eneo la Magomeni jijini Dar es Salaam iliyohusisha basi la Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka(Udart) maarufu kama Mwendokasi, lenye namba za usajili T 973 DGV na gari dogo aina ya Nissan March lenye namba T 968 DNZ.

Ajali hiyo ilitokea jana mchana eneo la Magomeni Mapipa jijini Dar es Salaam na kusababisha dereva wa gari ndogo kufariki dunia papo hapo.

Katika eneo la tukio basi hiyo liliharibika vibaya upande wa kushoto wa mlango wa mbele wa derava na kusababisha vioo vyote kuvunjika.

Gari ndogo iliharibika vibaya kwa kukatika vipande vipande huku dereva aliyekuwa akiendesha gari hilo ambaye inadaiwa alifariki dunia papo hapo baada ya kujeruhiwa vibaya.

Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Kipolisi Ilala, Mussa Taibu, alikiri kutokea kwa ajali hiyo na kusema kuwa, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa ndiye mwenye jukumu la kutoa taarifa hiyo.

Nipashe lilimtafuta Kamanda Mambosasa kupitia simu yake ya mkononi ambayo hata hivyo, iliita bila majibu.

Imeandikwa na Rose Jacob (Mwanza na Mary Geofrey (Dar).

 

Habari Kubwa