Ajali ilivyoua watano daraja lililobomoka

25Mar 2020
Ashton Balaigwa
Morogoro
Nipashe
Ajali ilivyoua watano daraja lililobomoka

JESHI la Polisi mkoani Morogoro linamsaka dereva Saidi Kifaila (30), anayedaiwa kutoweka baada ya gari alilokuwa anaendesha kusababisha ajali kwa kugonga magari matatu, likiwamo aina ya Noah, lililotumbukia korongoni na kusababisha vifo vya watu watano na kujeruhiwa wengine sita katika la ...

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa morogoro, Wilbroad Mutafungwa, picha mtandao

Daraja la Kiyegeya wilayani Kilosa.

Katika ajali hiyo, gari hilo aina ya Noah lenye namba za usajili T 403 DQP, lililokuwa linaendeshwa na Ramadhan Mohamed (28), lilisimama katika mteremko na magari mengine yaliyokuwa yakitokea Dar es Salaam na Morogoro kusubiri zamu yao kupita kwenye daraja hilo la mchepuko katika Barabara Kuu ya Morogoro- Dodoma.

Wakati magari hayo yakisubiri katika daraja hilo ambalo hivi karibuni lilibomoka kutokana na mvua kubwa, ghafla lori hilo lilikosa mwelekeo na kuligonga kwa nyuma gari aina ya Noah na kutumbukia nalo korongoni kwenye daraja hilo.

Imedaiwa na Jeshi la Polisi kwamba, Kifaila alikuwa akiendesha gari kubwa la mizigo aina ya FAW lenye namba za usajili T 623 DGY lenye tela T 233 BXZ, mali ya Kampuni ya Road Stell Haulage na alikuwa akitoka Dar es Salaam kwenda Dodoma.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Wilbroad Mutafungwa, alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo, akibainisha kuwa ilitokea Machi 22 mwaka huu majira ya saa 12 na nusu jioni maeneo ya Daraja la Kiyegeya katika Mto Mkange, tarafa ya Magole wilayani Kilosa.

Alidai dereva huyo, akiwa na gari hilo akitoka Dar es Salaam kwenda Dodoma, alipofika eneo hilo la daraja, breki za gari zilishindwa kuhimili na kukosa uelekeo na hivyo kuyapita magari ya mbele yake upande wa kushoto na hatimaye kuyagonga kwa nyuma magari matatu likiwamo aina ya Noah lililokuwa na abiria.

Mutafungwa alidai magari yote yalikuwa yakielekea upande wa Mkoa wa Dodoma na kwamba lori hilo lilikuwa limebeba shehena ya saruji.

Alisema watu wanne waliokuwa kwenye Noah wakitoka Dumila kwenda Gairo, walifariki dunia papo hapo na mmoja alifariki dunia wakati akipatiwa matibabu kwenye Kituo cha Afya cha St. Joseph Dumila na kwamba miili yao imehifadhiwa chumba cha maiti katika kituo hicho ikisubiri utambuzi wa ndugu.

Aliwataja waliofariki kwenye gari aina ya Noah kuwa ni Sijaona Chamene (29), mkulima na mkazi wa Kijiji cha Majawanga wilayani, Mahungo Martine (25), mkazi wa Gairo na wengine watatu ambao majina yao yalikuwa hayajatambuliwa, mmoja wao akiwa ni mwanamke.

Waliojeruhiwa kwenye Noah ni dereva Ramadhan Mohamed, mkazi wa Dumila, Eliwahad Mshana (28), mkazi wa Dumila, Mkoa Michael (25), mkulima na mkazi wa Gairo , Elimalek Msigula (28) na Neema Braiton (27), wote wakazi wa Pandambili wilayani Kongwa mkoani Dodoma.

Kamanda Mutafungwa alisema majeruhi walikuwa kwenye hali mbaya na waliwahishwa katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Morogoro kwa ajili ya matibabu zaidi.

Alisema mbali na kuparamia Noah, lori hilo pia liliyagonga magari mengine matatu yenye namba za usajili T 611 DHE aina ya Brevis, lililokuwa linaendeshwa na Makuka Robert (36), mkazi wa Manispaa ya Morogoro na gari lenye namba za usajili T 826 DCF Toyota Harrier, lililokuwa linaendeshwa na Manoro Martin (41), Mhasibu wa Utumishi na mkazi wa Dar es Salaam.

"Kwa sasa tunaendelea kumtafuta Kifaila ambaye ni dereva wa lori baada ya kukimbia mara tu ajali kutokea na kusababisha vifo vya watu na majeruhi," Kamanda Mutafungwa alisema.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Morogoro, Dk. Rita Lyamuya , alithibitisha kupokea majeruhi sita na kusema kuwa hali zao kiafya zilikuwa zinaendelea kuimarika baada ya kupatiwa matibabu.

Habari Kubwa