Ajali Scania, semi trela yaua watano

23Nov 2020
Lulu George
Handeni
Nipashe Jumapili
Ajali Scania, semi trela yaua watano

WATU watano wamefariki dunia na mmoja kujeruhiwa baada ya magari mawili kugongana na kuwaka moto, katika Kata ya Kitumbi wilayani hapa usiku wa kuamkia jana.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga,  Blasius Chatanda, amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kusema ilitokea juzi majira ya saa 5:00 usiku na kuhusisha gari lenye namba za usajili  T988 na tela lenye namba T 757 CGC aina ya Scania, lililokuwa likiendeshwa na Seleman Muya (32), mkazi wa Tanga.

Alisema gari hilo lilikuwa limepakia saruji kutoka Tanga kwenda Dodoma likiwa na abiria wawili ambao ni Bakari Tendwa mkazi wa Tanga na abiria mwingine ambaye hajafahamika majina yake.

Alisema gari lenye namba za usajili T 895 DMD aina ya Canter lililokuwa linaendeshwa na dereva aliyefahamika kwa jina moja la Rashid, akitokea Dar es Salaam kwenda Tanga akiwa na utingo wawili ambao wote wamefariki dunia.

Kamanda Chatanda alisema utingo hao waliofahamika kwa jina moja moja la Mujibu (28) na Dominic (20) wote ni wakazi wa Lushoto. 

"Baada ya magari kugongana yote mawili yaliwaka na kuteketea kwa moto na kusababisha vifo vya dereva na utingo wote waliokuwa kwenye canter pia kusababisha vifo kwa dereva wa semi na abiria mmoja ambaye hajafahamika. Majeruhi Bakari Tendwa ambaye ameungua moto kidogo maeneo ya kichwani na kuvunjika mguu wa kushoto,” alisema.

Kamanda Chatanda alisema majeruhi amelazwa Kituo cha Afya Mkata, huku miili ya marehemu ikiwa imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha kituo hicho kwa ajili ya utambuzi na uchunguzi wa daktari.

Alisema chanzo cha ajali hiyo ni dereva wa Canter kutaka kulipita gari lingine, wakati eneo hilo halifai kwa kupishana, hivyo kugongana na lori.

Habari Kubwa