Ajali ya Coaster yaua wawili, kujeruhi saba

09Aug 2016
Steven William
Muheza
Nipashe
Ajali ya Coaster yaua wawili, kujeruhi saba

WATU wawili wamekufa papo hapo na wengine saba kujeruhiwa baada ya basi dogo la abiria aina ya Coaster kugongwa kwa nyuma na basi la Tawaqal katika kijiji cha Kitopeni Wilaya ya Muheza mkoani Tanga.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Tanga, Leonard Paulo

Ajali hiyo ilitokea jana jioni.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Tanga, Leonard Paulo, akiwa eneo la tukio alisema kuwa ajali hiyo ilihusisha magari mawili ya abiria ikiwamo Coaster lenye namba za usajili T 289 DETA iliyokuwa ikitokea Lushoto kuelekea jijini Tanga na basi la abiria la Tawaqal lenye namba za usajili KCF 256 B aina ya Isuzu, lililokuwa likitoka jijini Dar es Salaam kuelekea Mombasa, Kenya.

Kamanda Paulo aliwataja watu waliokufa katika ajali hiyo kuwa ni Bakari Zumo na Ramadhani Bakari, mkazi wa Kerenge wilayani Muheza.

Hata hivyo, alisema majina ya majeruhi ambao hali zao ni mbaya na wamelazwa katika Hospitali Teule ya Muheza, bado hayajafahamika.

Aidha, alimtaja dereva wa basi la Tawaqal kuwa ni Hemed Jamal na wa basi dogo la Coaster amefahamika kwa jina moja la Innocent.

Kamanda Paulo alisema chanzo cha ajali hiyo baada ya basi aina ya Coaster kufunga breki gafla ili kuchukua abiria sehemu isiyo na kituo eneo hilo la Kitopeni na kusababisha basi la Tawaqal lililokuwa nyuma yake, kuligonga na kusababisha vifo hivyo na majeruhi.

Mganga Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Elias Mayalla, alithibitisha kupokea maiti mawili pamoja na majeruhi saba wa ajali hiyo.