Ajali ya Noah, lori ilivyoua watano

04Jul 2020
Paul Mabeja
Dodoma
Nipashe
Ajali ya Noah, lori ilivyoua watano

WATU watano wamekufa na wengine wawili kujeruhiwa katika ajali ya barabarani iliyohusisha gari aina ya Noah lenye namba za usajili T 897 DCC na lori aina ya Scania lenye namba za usajili T 183 AXC.

Wananchi wakishuhudia mabaki ya gari aina ya Noah yenye namba za usajili T 897 DCC, baada ya kugongana na Lori aina ya Scania lenye namba za usajili T183 AXC, katika eneo la Kibaigwa wilayani Kongwa, mkoani Dodoma jana, na kusababisha watu watano kufariki dunia na wawili kujeruhiwa. PICHA: PAUL MABEJA

Ajali hiyo ilitokea jana majira ya saa 11:30 alfajiri eneo la Kibaigwa wilayani Kongwa mkoani Dodoma.

Akizungumza na waandishi wa habari jana katika eneo la tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto, alisema chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa lori aliyeingia barabarani bila kuchukua tahadhari.

“Mpaka sasa ninapozungumza, tayari watu watano wamepoteza maisha, akiwamo dereva wa gari dogo aina ya Noah, Yohana Ndugai, (34), na wengine wawili ni majeruhi, ambapo mmoja wao yuko mahututi,” alisema.

Kamanda Muroto alisema dereva wa lori aina ya Scania lililokuwa likitokea Dodoma kwenda Morogoro, ndiye mwenye makosa kutokana na kuingia barabarani bila kuchukua tahadhari, na kwamba mara tu baada ya kutokea kwa ajali hiyo, alikimbia na Jeshi la Polisi linaendelea kumtafuta.

“Huyu dereva, yeye alitumwa kuja huku Dodoma kuleta ‘spea’, lakini kutokana na tamaa, alipakia na watu wengine kama abiria ambao baadhi yao ndiyo wamehusika katika ajali hii.

"Hivyo basi, nitoe wito kwa madereva kuhakikisha kuwa wanazingatia sheria za usalama barabani," Kamanda Muroto alisema.

Alisema Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma litaongeza usimamizi mkali kwa madereva wote wanaovunja sheria hasa katika kipindi hiki ambacho Mkoa wa Dodoma, unakwenda kupokea wageni wengi kwa ajili ya mkutano mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mwezi huu.

“Ninafikiria sasa madereva wameshaanza kuleta uzembe ambao tulikuwa tunaupigia kelele, kwa sababu katika ajali hii huyu dereva ameingia bila kuchukua tahadhari na pia hajaheshimu gari lingine kutokana na yeye kuwa na lori kubwa, ndiyo maana hakumheshimu mwenye Noah," alisema.

Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Deogratius Ndejebi, akiwa katika tukio hilo, alisema: “Tunashukuru Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma, kwa kazi waliyoifanya kwani wamefika katika eneo la tukio kwa wakati, hali ambayo imesaidia hata barabara hii kuendelea kupitika pamoja na kuwa lori hili baada ya kupata ajali, liliziba sehemu ya barabara," alisema.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Binilith Mahenge, akizungumza katika ajali hiyo, alilitaka Jeshi la Polisi kuendelea kumtafuta dereva wa lori aliyesababisha ajali hiyo na kukimbia.

“Lakini pia nitoe angalizo kwa madereva kuhakikisha kuwa wanakuwa makini wakati wote wanapoendesha vyombo vya moto, kwani wamepakia roho za binadamu, ni lazima wawe makini kila wakati ili kuondokana na uzembe kama huu," aliagiza.

Kiongozi huyo wa mkoa pia aliwaagiza wakurugenzi wa Wilaya za Chamwino, Kongwa na Bahi, kuhakikisha malori yote yanayoegeshwa katika maeneo ya barabara, yanaacha kufanya hivyo mara moja.

"Tulikubaliana katika kikao cha ushauri mkoa (RCC) kuwa katika eneo la Kibaigwa, Chalinze nyama na Bahi malori hayatakiwi kuendelea kuegeshwa katika maeneo ya barabara, bali wakurugenzi watafute maeneo maalum kwa jili ya kuegesha malori, ili kuondokana na ajali kama hizi za kizembe," alikumbusha.

Habari Kubwa