Ajali yaua maofisa 5 wa serikali

22Oct 2018
Na Mwandishi Wetu
Manyoni
Nipashe
Ajali yaua maofisa 5 wa serikali

WAFANYAKAZI watano wa Wizara ya Kilimo, wamefariki dunia baada ya gari walilokuwa wakisafiria kupata ajali jana eneo la Manyoni, mkoani Singida.

Kwa mujibu wa taarifa iliyothibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Sweetbet Njewite, maofisa hao walikuwa katika gari aina ya Mitsubishi Pajero, wakitokea Dodoma kuelekea Shinyanga.

Kamanda Njewite alieleza kuwa gari hilo lilikuwa limewabeba maofisa wanne wa Wizara ya Kilimo pamoja dereva ambao wote walifariki hapo hapo.

Alisema gari hilo liliacha njia ghafla na kupinduka eneo la Manyoni majira ya saa tano asubuhi.

"Bado tunachunguza chanzo cha ajali hiyo, lakini ninachoweza kuthibitisha kuwa ni gari la Wizara ya Kilimo na walikuwa wanatokea jijini Dodoma kuelekea mkoani Shinyanga kikazi," alisema Kamanda Njewite.

Kamanda Njewite alieleza kuwa baada ya kutokea kwa ajali hiyo maofisa hao walikimbizwa katika Hospitali ya Manyoni, lakini iligundulika kuwa walikuwa wameshafariki eneo la tukio.

Alisema kuwa kwa sasa miili ya marehemu hao imehifadhiwa katika Hospitali ya Singida mjini ili kusubiri taratibu zingine za mazishi.

Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, ilitaja waliofariki katika ajali hiyo kuwa ni Stella Ossano (39), Ester Mutatembwa (36), Abdallah Mushungusi (53), Charles Somi na Erasto Mhina (43).

Taarifa ilisema miili ya marehemu iko njiani kuelekea Hospitali ya Dodoma.

Kufariki kwa maofisa hao kunafanya idadi ya ajali za maofisa wa wizara nchini zilizotokea ndani ya miezi sita kuwa nne.

Ajali ya kwanza ilitokea Mei 22, maofisa watatu wa Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC), walifariki dunia baada ya gari walilopanda kupata ajali eneo la Chalinze wakiwa njiani kuelekea Dodoma.

Kadhalika, Julai 30, mwaka huu maofisa wawili wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, akiwamo Ofisa Habari wa wizara hiyo, Shadrack Sagati, walifariki baada ya gari walilokuwamo kupinduka wilayani Chato, mkoani Geita.

Aidha, Agosti 4, mwaka huu gari la Wizara ya Maliasili na Utalii, lilipata ajali eneo la Manyara na kusababisha kifo cha Ofisa Habari wa wizara hiyo, Hamza Temba, pamoja Waziri wa Wizara hiyo, Khamis Kigwangala kujeruhiwa vibaya.