Ajali zamshitua Magufuli

22Sep 2016
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Ajali zamshitua Magufuli

RAIS John Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella kufuatia vifo vya watu 13 vilivyosababishwa na ajali ya barabarani jana

ikiwa ni siku moja tu baada ya Mkuu wa Nchi huyo kufanya hivyo kwa Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Dk. Rehema Nchimbi kutokana na ajali ya basi iliyoua watu 12 mkoani humo Jumatatu usiku.

Taarifa iliyotolewa jana na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ilulu, ilieleza kuwa ajali ya jana ilitokana na basi la abiria la kampuni ya Super Shem kugonga daladala aina ya Toyota Hiace katika kijiji cha Mwamaya kilichopo katika kata ya Hungumalwa wilayani Kwimba mkoani Mwanza.

Ilieleza kuwa ajali hiyo ilitokea majira ya saa 12:15 asubuhi baada ya basi hilo dogo lililokuwa likitoka kijiji cha Shirima kwenda Nyegezi mjini Mwanza, kuingia ghafla barabara kuu kisha kugongwa na basi hilo lililokuwa likitoka mkoani Mbeya kwenda Mwanza.

Taarifa hiyo ilifafanua kuwa Rais ameelezea kupokea taarifa za ajali hiyo kwa mshituko mkubwa hasa ikizingatiwa kuwa imetokea ikiwa ni siku moja tu tangu Watanzania wengine 12 wapoteze maisha katika ajali ya basi la kampuni ya New Force iliyotokea katika kijiji cha Lilombwi, kata ya Kifanya, tarafa ya Igominyi mkoani Njombe.

Nimesikitishwa sana na vifo vingine vya Watanzania wenzetu waliopoteza maisha katika ajali huko Mwanza, nakuomba Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella unifikishie salamu za pole kwa familia zote zilizopoteza ndugu, jamaa na marafiki katika ajali hii.

Nawaombea wote waliotangulia mbele za haki wapumzishwe mahali pema na pia wote walioguswa na msiba wawe na moyo wa subira, uvumilivu na ustahimilivu katika kipindi kigumu cha majonzi ya kuondokewa na jamaa zao," ilisomeka taarifa hiyo ikimnukuu Rais Magufuli.

Taarifa zaidi kutoka jijini Mwanza zilieleza kuwa basi hilo liligonga daladala katika makutano ya barabara kuu ya kutoka Shinyaga na Misasi wilayani Kwimba na kusababisha vifo vya watu 13 na kujeruhi 15, watatu kati yao walikuwa katika hali mbaya na walipelekwa Hospitali ya Rufaa Bugando. Basi hilo lenye namba za usajili T 874 CWE na Hiace yenye namba za usajili T 368 CWQ, yalidaiwa kuwa katika mwendokasi na kwamba watu 10 walifariki dunia papo hapo baada ya basi kuigonga daladala, huku watatu wakipoteza maisha wakati wakipelekwa hospitali.

Akizungumza mbele ya Mongella, Mkuu wa Wilaya ya Kwimba, Mtemi Msafiri alisema kwa mujibu wa taarifa alizopewa na Mganga Mfawidhi wa Hospital ya Wilaya ya Kwimba, Benson Mchemba, miili tisa ya marehemu imetambuliwa huku mitatu, ukiwamo wa mtoto anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka mitatu hadi minne, ilikuwa haijatambuliwa mpaka jana mchana.

Alisema miili miwili ya marehemu imehifadhiwa katika hospitali hiyo na mmoja uko kwenye Hospitali ya Wilaya ya Misungwi.

Msafiri aliyataja majina ya marehemu waliotambuliwa kuwa ni Monica Shija, Constatine Emmanuel, mtoto wa Monica Shija, Lwinzi Cope, Mabula Magi, Poni, Theresa Majenga, Issaya Deogratius, Mosses Kame. Alisema miongoni mwa miili hiyo, wamo watoto wawili wenye umri chini ya miaka mitano.

Kiongozi huyo wa serikali ya wilaya alisema majeruhi waliotambulika kwa majina yao ni Antony Shilima ambaye ni dereva wa basi, Faustine Emmanuel ambaye ni kondakta wa daladala, Shija Loketi (abiria) na mtoto aliyetambulika kwa jina moja la Martin.

Alisema majeruhi wengine walishindwa kuwatambua kwa majina yao kutokana na kuwa katika hali mbaya, kiasi cha kushindwa kuzungumza.

Mongella alifika kwenye eneo ilipotokea ajali pamoja na hospitali zote mbili akiwa na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya na mkoa.

Niwape pole wale wote walifikwa na matatizo haya, inatia uchungu kuona madereva wanafanya uzembe katika maisha ya watu na kupelekea vifo vinavyoweza kuzuilika,alisema Mongella.

Serikali haitokubali kuona uzembe huu ukiendelea, lazima hatua kali zichukuliwe dhidi ya madereva wazembe.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Hamed Msangi alisema kutokea kwa ajali hiyo katika kipindi hiki cha wiki ya Nenda kwa Usalama, kunawapa changamoto ya kuhakikisha elimu ya kutosha kwa madereva inatolewa.

MKEMIA MKUU
Wakati ajali za barabarani zikiendelea kugharimu maisha ya watu na kupoteza nguvu ya taifa, Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali imesema ipo kwenye hatua za mwisho za kuanzisha kitengo cha kupima madereva wanaosafirisha mizigo ili kubaini aina ya vilevi wanavyotumia.

Mkemia Mkuu wa Serikali, Profesa Samwel Manyele aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akifungua mafunzo kwa wadau wa kemikali, wakiwamo madereva wanaosafirisha, watunzaji na watumiaji yenye lengo la kuwapa uwezo na uelewa na namna ya kukabiliana matukio au ajali.

Alisema lengo la kuanzisha mpango huo maalum wa kudhibiti ajali za barabarani ni kubaini aina ya kilevi wanachotumia madereva na kusababisha ajali zinazogharimu maisha ya watu.

Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali ipo kwenye hatua za mwisho za kukamilisha utaratibu huo mpya wa kupima madereva wote wanaosafirisha mizigo ikiwamo kemikali na tutabaini chanzo kimoja kimoja cha ina ya kila kilevi wanachotumia madereva kutumia mfumo huo,; alisema Prof. Manyele.

Alisema chanzo kikubwa cha ajali nyingi za barabarni ni ulevi, ofisi yake itafanya kazi ya kubaini aina ya kilevi wanachotumia ili kukabiliana na madhara yanayotokana na ajali hasa za kemikali.

Prof. Manyele alisema kutokana takwimu za ajali za barabarani zinazoripotiwa za watu tisa kupoteza maisha kila siku, zinaitia shaka usalama wa madereva hivyo watahakikisha wanashirikiana na wakaguzi wa barabarani kukagua aina ya vilevi wanavyotumia.

Mbali na hilo, alisema katika kipindi cha mwaka 2014 jumla ya matukio na ajali za kemikali zilizotokea ni 11 zilizosababisha vifo vya watu 14, uharibufu wa mali, ikiwamo zaidi ya tani 250 za kemikali kuungua kwa moto, madhara ya kiafya na mazingira.

Alisema kwa mwaka 2013, matukio yalikuwa nane yaliyosababisha madhara kwa watu tisa na kwamba chanzo kikuu cha matukio hayo ni uelewa mdogo wa watumiaji wa kemikali. Alisema ili kuondokana na madhara yanayotokana na matumizi yasiyo salama ya kemikali, serikali iliamua kutunga Sheria ya Kemikali za Viwandani na Majumbani Na. 3 ya Mwaka 2003.

Alisema lengo la sheria hiyo ni kuhakikisha kuwa kemikali zinatumika katika hali iliyosalama bila kuleta athari kwa watu na mazingira na kwamba kabla ya sheria hiyo, kemikali zilikuwa zikiletwa nchini kiholela na kutumika bila ufuatiliaji. Pia alisema mafunzo hayo yataendelea kutolewa kwa makundi mbalimbali ya watumiaji wa kemikali ili kujikinga dhidi ya matumizi ya hatari ya madhara yatokanayo na ajali za kemikali.

Habari Kubwa