Ajeruhiwa vibaya kwa kugonga nyati

15Jan 2022
Idda Mushi
Morogoro
Nipashe
Ajeruhiwa vibaya kwa kugonga nyati

THOBIAS Mbilinyi (47), mkazi wa Makambako mkoani Njombe amejeruhiwa vibaya baada ya gari alilokuwa akisafiria kugonga wanyamapori wawili aina ya nyati waliofariki dunia papo hapo katika eneo la tukio, ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Mikumi, barabara kuu ya Morogoro-Iringa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Fotunatus Muslim, alithibitisha juzi kutokea kwa ajali hiyo ambapo Mbilinyi alijeruhiwa vibaya huku nyati wawili dume wakifariki dunia katika ajali iliyotokea Januari 10, majira ya  saa 1:00 asubuhi.

Alisema ajali hiyo imehusisha gari  dogo aina ya Toyota Crown  lenye namba za usajili T 995 DLF lililokuwa likiendeshwa na Mbilinyi, likitokea Dar es Salaam kwenda Makambako na chanzo ni mwendo kasi wa dereva.

"Ndani ya hifadhi uendeshaji ni kilometa 70 kwa saa mchana na usiku ni kilometa 50 kwa saa, lakini dereva hakufuata taratibu na kusababisha ajali hii" alisema SACP Musilim.

Akabainisha kuwa majeruhi wa ajali hiyo alipelekwa kituo cha Afya Mikumi, baadaye Hospitali ya  Rufaa ya Mkoa wa Morogoro alikopewa rufaa kwenda Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kutokana na majeraha makubwa aliyopata  hasa sehemu za kichwa na shingoni.

Kamanda huyo wa Polisi alisema mtuhumiwa huyo akiruhusiwa kutoka hospitali anatarajiwa kufikishwa mahakamani kujibu mashtaka yanayomkabili.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufani ya Morogoro, Dk. Daniel Nkungu, alithibitisha kumpokea majeruhi huyo majira ya saa 5:00 asubuhi akitokea Mikumi na alikuwa ameumia sana maeneo ya usoni na shingoni. Alisema baada ya huduma ya kwanza ya  dharura iliyochukua karibu muda wa saa moja, alisafirishwa kwenda Muhimbili.

Naye  Kaimu Mhifadhi wa Hifadhi ya Taifa ya Mikumi, Herman Mtei,  alisema nyati hao wawili waliogongwa, kila mmoja ana thamani ya Dola za Kimarekani 1,900 na kwamba mtuhumiwa atapewa adhabu mbalimbali  kulingana na tukio hilo.

"Adhabu ambazo mtuhumiwa atalazimika kulipa ni pamoja na faini ya uchafuzi wa mazingira katika hifadhi ya Sh. 50,000, faini ya mwendokasi Sh. 50,000, faini ya kusababisha ajali hifadhini Sh. 200,000 na faini ya kugonga nyati kila mmoja atalazimika kulipa Dola za Kimarekani 1,900,"alisema Mtei.

Hifadhi ya Mikumi inakatizwa na barabara kuu ya Morogoro-Iringa, jambo linalosababisha vifo kwa wanyama, uchafuzi wa mazingira na wapita njia kubadilisha tabia za wanyama kwa kuwalisha wanyama vyakula vinavyotumiwa kibinadamu na utalii wa bure kwa wapita njia.

Hata hivyo Serikali kwa kuliona hilo ilianza mchakato wa ujenzi wa kiwango cha lami kwa barabara ya Turiani-Magole-Dumila-Rudewa-Kilosa hadi Mikumi ili pamoja na mambo mengine, iondoe ulazima uliopo sasa wa watumiaji wa magari kukatiza bure ndani ya hifadhi hiyo.

Habari Kubwa