Ajifungua, amuua mtoto na kumfukia shimoni

22Jun 2016
Marco Maduhu
Shinyanga
Nipashe
Ajifungua, amuua mtoto na kumfukia shimoni

MARIAMU Shabani (21), mkazi Wilaya ya Kahama mkoani hapa, anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kujifungua mtoto na kumuua kwa kumfukia shimoni.

Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Shinyanga, Mika Nyange

Mwanamke huyo ambaye ni muhudumu wa baa, alidaiwa kutenda unyama huo, Juni 18, mwaka huu, mara baada ya kujifungua katika nyumba aliyokuwa akiishi.

Hata hivyo, majirani waliugundua ‘mchezo’ uliofanywa na mwanamke huyo baada ya kujaribu kumuokoa mtoto huyo kutoka shimoni na kumkimbiza hospitalini, lakini alifariki dunia muda mfupi baadaye.

Akizungumza na Nipashe juzi kwa niaba ya Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Shinyanga, Mika Nyange, Mrakibu mwandamizi wa polisi mkoani humo, Graphton Mushi, alisema baada ya kutokea kwa tukio hilo, polisi ilifanikiwa kumshikilia mwanamke huyo kwa kosa la mauaji.

Mushi alisema mwanamke huyo anatarajiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote kujibu shitaka linalomkabili ili liwe fundisho kwa wazazi wengine wenye tabia kama hiyo pia kukomesha mauaji ya kikatili mkoani humo.

Aidha, katika tukio jingine polisi mkoani humo, inamshikilia, Balele Zanzibar, mkazi wa Songwa, wilayani Kishapu kwa kosa la kumuozesha mtoto wake mwanafunzi wa darasa la sita, baada ya kupokea ng’ombe 14.

Kamanda Mushi alisema ndoa hiyo ilitibuliwa Juni 18, baada ya kumkamata mzee huyo pamoja na muoaji, kwa kushirikiana na Shirika la kutetea haki za watoto (Agape).

“Baada ya kufika eneo la tukio tulikuta ndoa ya kimila ikifungwa, hivyo tukawakamata baba wa motto huyo pamoja na muoaji, Sena Sungwa, mkazi wa Maswa mkoani Simiyu kwa kosa la kuoa mwanafunzi jambo ambalo ni kosa kisheria,” alisema Mushi.

Habari Kubwa