Ajinyonga hadi kufa kwa kutotajwa misa ya shukrani

06Dec 2021
Elizabeth John
Njombe
Nipashe
Ajinyonga hadi kufa kwa kutotajwa misa ya shukrani

WATU wawili wamefariki dunia katika matukio tofauti, likiwamo la mmoja kujinyonga baada ya kutotajwa kanisani kwenye misa ya shukrani na mwingine kukatwa mapanga kichwani na kufumuliwa fuvu baada ya kutoa ushahidi katika kesi ya migogoro ya ardhi.

Kamanda wa Polisi Mkoani wa Njombe Hamisi Issah.

Katika tukio la kujinyonga, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Hamisi Issah amesema, Ravan Lazaro (48), mkazi wa Ludewa, mtaa wa Kanisani B amejinyonga kwa waya kwa kile kinachodaiwa kutotajwa katika misa ya shukrani kanisani.

Kamanda Issah amesema mtu huyo na mkewe walikuwa na mtoto mwenye umri wa miaka 10 ambaye alivunjika mguu na baada ya kutibiwa hospitali na kupona walienda kanisani kutoa shukrani.

"Wakati wa shukrani padre wa kanisa alimtaja mama wa mtoto peke yake bila kumtaja baba hali iliyoleta sintofahamu na matokeo yake ameamua kujinyonga kwa kutumia waya," amesema.

Kamanda Issah amewataka viongozi wa dini kuzingatia umuhimu wa familia kwa kuwa inajumuisha baba na mama, akitajwa mmoja matokeo yake inaleta hali kama hiyo.

Aidha, aliyeuawa kwa kufumuliwa fuvu ametambuliwa kuwa ni Daudi Kivavala (70), mkazi wa Kijiji cha Udonja, Wilaya Wanging'ombe, mkoani Njombe.

Kamanda Issah amesema tukio hilo lilitokea Desemba 5, mwaka huu saa 11:30 jioni.

Amesema Kivavala, alikuwa akiyafahamu maeneo mbalimbali ya kifamilia na alitakiwa kutoa ushahidi kwa Mwenyekiti wa kitongoji ili kumaliza mgogoro wa kifamilia, ambao hata hivyo, wanafamilia hao walionekana kutoridhika na ushahidi huo.

"Baada ya ushahidi huo kuna sintofahamu ya baadhi ya wanafamilia kutokuridhika…shahidi huyu ameuawa kwa kukatwa mapanga sehemu za kichwani mpaka fuvu limetoboka, jambo hili linasikitisha sana tusingependelea, tunasema kabisa migogoro mingi ambayo haina utatuzi inawezekana mashahidi wanapotea kwa njia kama hii iliyotokea," amesema Kamanda Issah.

Amewataka wananchi kuridhika na uamuzi unaotolewa na viongozi wenye dhamana badala ya kujichukulia sheria mkononi.

"Mkiwa na maamuzi yenu tofauti ndiyo matukio haya yanaweza yakatokea, shahidi muhimu amekuja kutoa ushahidi na haki itendeke na baadaye amepoteza maisha," amesema.

Habari Kubwa