Ajinyonga kukimbia deni la mkopo alioudhamini

16Jul 2017
Marco Maduhu
Nipashe Jumapili
Ajinyonga kukimbia deni la mkopo alioudhamini

SARAH Bundala (55), mkazi wa mtaa wa Tambukareli Shinyanga mjini, amefariki dunia kwa kile kilichodaiwa kuwa ni kujinyonga baada ya kushindwa kurejesha mkopo.

Aidha, inadaiwa mkopo huo si wake bali alikuwa amemdhamini rafiki yake aliyetoroka na pesa hizo ambazo, hata hivyo kiasi chake hakikufahamika.

Ndugu zake walidai kuwa Sarah alimwita rafiki yake Mariamu Mugaya, saa 8:00 mchana juzi ili amsindikize mtaani kwa jamaa zao wakatafute pesa za kulipa mkopo huo anatakiwa aurejeshe.

Hata hivyo, walipozunguka na kukosa wa kuwasaidia ndipo akamshauri ampigie simu mumewe kumuomba amsaidie Shilingi 40,000 anazohitaji, lakini naye akagoma kumpigia.

Alisema baada ya kushauriana wapi watapata pesa na kukosa majibu, Sarah alimwambia aenda nyumbani, ili naye akalale muda na ikifika saa 10 jioni, aje nyumbani kumwona. Alimweleza kuwa hata watu wakimuuliza yuko wapi awaambie amelala nyumbani kwake asiwafiche.

Mariama alisema cha kushangaza ilipofika muda huo akapokea taarifa kuwa rafiki yake amejinyonga.

Mume wa marehemu Sarah, Laurent Mabina, alisema alipokuwa kazini saa 9:00 mchana alipigiwa simu na mke wake huyo akimuomba Shilingi 40,000, lakini hakutaka kumuuliza ni za nini, bali alimjibu atakuja nyumbani kumalizana naye.

Aliporudi na kuingia chumbani akamkuta mke ameshajinyonga.

Alisema chanzo hakukifahamu lakini baada ya kudodosa akagundua kuwa ni mikopo, ambayo awali walikopa pesa wakashindwa kurejesha.

Alisema kuna wakati alikopa akashindwa kurejesha na ikamulazimu azilipe na kumzuia kukopa tena, lakini akafanya siri kwenda kumdhamini rafiki yake bila kujua kuwa amemtoroka.

“Kilichomsababishia mke wangu kufikia hatua ya kujinyonga, ni ile hofu kuwa nikirudi nyumbani nitakuja kumgombeza, sababu nilishamkataza kujiingiza kwenye mikopo, na baada ya kushindwa sasa kurejesha hayo marejesho ya mkopo wa rafiki yake aliyetoroka, akaona heri ajinyonge,”alilalamika Mabina.

Kwa upande wake Kamanda wa Jeshi Mkoa wa Shinyanga Jumanne Muliro, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kubainisha hakuna mtu yeyote anayeshikiliwa.

Alisema mwanamke huyo alijiua mwenyewe na mwili wake umehifadhiwa kwenye hospitali ya mkoa wa Shinyanga.

Habari Kubwa