Ajira 50,000 zaja utumishi wa umma

17Apr 2018
Sanula Athanas
DODOMA
Nipashe
Ajira 50,000 zaja utumishi wa umma

SERIKALI imesema inatarajia kuajiri watumishi wapya 49,356 katika mwaka ujao wa fedha utakaoanza Julai.

Kapteni mstaafu George Mkuchika.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapteni mstaafu George Mkuchika, ndiye aliyetoa kauli hiyo jana bungeni mjini hapa alipokuwa anahitimisha hoja ya makadirio ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2018/19.

Alisema ajira katika utumishi wa umma hutegemea bajeti ya serikali, hivyo itakaporuhusu, ajira kiasi hicho zimepangwa kutolewa.

Akifafanua kuhusu ajira hizo, Mkuchika alisema walimu shule za msingi na sekondari ni 16,000, kada ya afya nafasi 15,000 na nafasi zilizobaki zitakuwa ni kwa ajili ya kada nyingine zikiwamo kilimo, uvuvi, mifugo, vyombo vya ulinzi, magereza, uhamiaji, watendaji na wahadhiri.

Mkuchika ambaye pia ni Mbunge wa Newala, alibainisha kuwa hadi kufikia Machi 31, mwaka huu, serikali ilikuwa imeajiri watumishi zaidi ya 18,000 kuziba maeneo yenye upungufu mkubwa wa watumishi wa umma.

Alisema katika mwaka huo uliobakisha siku 73 kufika ukomo, walipanga kuajiri watumishi 52,000 ambao wengi wao ni wa idara ya elimu, afya na serikali za mitaa.

“Hawa tunaowaajiri mmeshawapitisha katika bajeti iliyopita, ni tofauti na 49,356 tutakaowaajiri mwaka wa fedha 2018/19,” alisema.Mkuchika alisema ni vyema Watanzania wakafahamu kuwa zoezi la kuajiri lilisimama wakati wa kuhakiki vyeti vya taaluma na kitaalamu vya watumishi wa umma, akieleza kuwa uhakiki huo umeshakamilika.

Alisema tayari serikali imeajiri watumishi mbadala wa walioondolewa, zoezi ambalo alisisitiza ni karibu linakamilika na hivyo wataendelea na ajira mpya.

“Kama ilivyo kwa suala la ajira, upandishaji wa vyeo hutegemea sifa za muundo wa utendaji mzuri na bajeti ya mishahara,” alisema.Waziri huyo alisema serikali katika mwaka ujao wa fedha imetenga nafasi 162,221 kupandisha vyeo kwa watumishi wenye sifa stahiki wa kada mbalimbali.

Alisema katika nafasi hizo, 2,044 zimetengwa kwa ajili ya kuziba mapengo mbalimbali kwa ajili vyeo katika ngazi ya madaraka.“Uteuzi huu utapunguza nafasi za kukaimu. Natoa rai kwa mamlaka za ajira na mamlaka nyingine zinazohusika kuhakikisha kuwa zinaanzisha mchakato mapema kwa kuzingatia vigezo vya miongozo mbalimbali.” 

Akizungumzia hoja ya nyongeza ya mshahara iliyochangiwa na wabunge wengi wakati wa mjadala wa makadirio ya bajeti ya wizara yake, Mkuchika alisema ni suala la kibajeti.

Hata hivyo, waziri huyo alisema serikali inakusudia kutoa nyongeza ya mwaka kwa mujibu wa Kanuni za Utumishi wa Umma.

KUTEKWA, KUPIGWA

Mkuchika pia alifafanua kuhusu kile alichokiita malalamiko ya wabunge kuhusu kutekwa, kupigwa watu na upendeleo mwingi kwa chama tawala, akieleza kuwa serikali haiungi mkono mambo hayo na ndiyo maana yanapojitokeza huchukua hatua mara moja.

“Jeshi lenye dhamana na usalama wa raia ni Jeshi la Polisi na si Idara ya Usalama wa Taifa. Natoa wito kwa wananchi kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi ili waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo,” alisema.

Waziri huyo pia alizungumzia madai ya kukiukwa kwa Katiba ya nchi kutokana na kuzuia mikutano ya hadhara, wanaokosoa serikali kupata mateso na wengine kupotea na viongozi wa dini kupata misukosuko, akisema serikali haikiuki Katiba katika utekelezaji wa shjughuli zake.

“Taasisi yoyote inayoona inanyimwa haki yake kikatiba ina nafasi ya kupeleka mamalamiko yake katika vyombo vinavyotoa haki ambayo ni mahakama,” alisema.

Aliongeza kuwa serikali haina ushahidi wa viongozi wa dini kupata misukosuko na hapendi kulichangia suala hilo.

“Niseme kifupi, ukitaka kumshauri mzee wako huitishi mkutano wa hadhara... hakuna, njia ya kumfikia baba yako (ni) kimyakimya,” alisema Mkuchika.

Kuhusu malalamiko ya wabunge juu ya kuwekwa ndani kwa watu kwa zaidi ya saa 24 kunakofanywa na baadhi ya wakuu wa mikoa na wilaya, Mkuchika alisema Sheria ya Utawala ya mwaka 1997 imewapa viongozi hao mamlaka ya kuwaweka ndani watu saa 24 kama wanabainika kutenda kosa lolote lenye kuhatarisha amani na utulivu kwa jamii.

“Anayeona hakutendewa haki kwa misingi ya sheria hiyo anayo haki ya kulalamika kwa wakubwa wake wa kazi na kama hakuridhika, ruksa kwenda mahakamani,” alisema.

Kuhusu Diwani wa Kakongo (CCM) aliyepotea, Mkuchika alisema hawapuuzi kupotea kwa watu nchini na kwamba uchunguzi unaendelea kuhusiana na tukio hilo baada ya kuripotiwa kwa Jeshi la Polisi.

Habari Kubwa