Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera na Uratibu wa Bunge, George Simbachawene, alibainisha hayo jana alipokuwa akitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu kuanza mchakato wa ajira za makarani na wasimamizi wa sensa.
“Kwa niaba ya mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Kamati ya Taifa ya Sensa, napenda kutangazia Watanzania wenye sifa na wenye kuhitaji kuomba nafasi hizi kwamba mchakato wa kuwapata makarani na wasimamizi wa sensa utaanza leo (jana) tarehe 5 hadi tarehe 19 Mei, 2022.
“Nipende kuweka wazi kwamba ajira hizi zitaombwa kupitia mtandao (Online) na hazitahusisha malipo ya aina yoyote kwa mwombaji wa ajira,” alisisitiza Simbachawene.
Alisema mchakato wa kuchambua maombi ya kazi pamoja na usaili utasimamiwa na kamati maalum itakayoundwa katika ngazi ya kila wilaya na usaili utafanyika katika ngazi ya kata kwa nafasi za makarani na wasimamizi wa maudhui katika ngazi ya wilaya kwa wasimamizi wa TEHAMA.
“Niwaombe Watanzania wote wenye sifa ambao wangependa kuomba nafasi za ajira za makarani na wasimamizi wa sensa kufuata utaratibu uliowekwa kwa ukamilifu ili kuomba nafasi hizo,” alisema.
Kadhalika, alisema kazi za kufanya pamoja na sifa za mwombaji zimebainishwa katika tangazo la ajira za muda za makarani na wasimamizi wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022.
“Hakutakuwa na maombi yatakayofanyiwa kazi zaidi ya yale yatakayofuata utaratibu uliowekwa mtandaoni.
“Kumekuwapo na watu au makundi ya watu wenye nia isiyo njema kwa zoezi la sensa ambao wamekuwa wakijaribu kutoa matangazo ya ajira hizo kwa nia ya kuwatapeli wananchi wanaohitaji kushiriki katika zoezi hili na pengine kwa nia ya kuvuruga mchakato mzima serikali itaendelea kuwafuatilia na kuwachukulia hatua kali watu wote wenye nia ovu ya kuharibu zoezi hili,” alisema.
Pia, alisema kutokana na hali hiyo serikali imetangaza rasmi kuanza kwa mchakato wa ajira za makarani na wasimamizi kuanzia jana hadi Mei 19, mwaka huu, ambao utahusisha wasimamizi wenye sifa stahiki na watakaofanya kazi katika maeneo yao wanayoishi.
Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi mwaka 2022 na Spika mstaafu wa Bunge, Anne Mkinda alisema maandalizi ya zoezi hilo yamekamilika kwa asilimia zaidi ya 81.
“Maandalizi kwa ujumla yamekamilika kwa takribani zaidi ya asilimia 81 na hivi sasa tumetangaza ajira hizi za makarani na wasimamizi wa sensa ya watu na makazi hivyo wito wangu kwa Watanzania wenye sifa kujitokea kuomba kwani tukipata makarani wasio na sifa zoezi zima litaharibika,” alisema Makinda.