Ajira, serikali kuhamia Udom mtego kwa Waziri Ndalichako

06Mar 2017
Sanula Athanas
Dar es Salaam
Nipashe
Ajira, serikali kuhamia Udom mtego kwa Waziri Ndalichako

KATIKA uchambuzi huu Ijumaa iliyopita, ilielezwa jinsi Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene na msaidizi wake, Selemani Jafo, wanavyokabiliwa na mtihani mgumu kutekeleza bajeti ya wizara yao kwa mwaka huu wa fedha.

Waziri Prof. Joyce Ndalichako.

Zikiwa zimebaki siku 116 kabla ya kufika kikomo kwa mwaka wa fedha 2016/17 na siku 29 kabla ya kuanza kwa Bunge la Bajeti ya serikali kwa mwaka ujao wa fedha, leo katika mwendelezo wa uchambuzi huu tunaiangalia Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi inayoongozwa na Waziri Prof. Joyce Ndalichako akisaidiwa na Mhandisi Stella Manyanya.

Kwenye uongozi wao wizarani hapo, Prof. Ndalichako na Mhandisi Manyanya, wamefanya vizuri katika kushughulikia dosari zilizokuwapo katika udahili wa wanafunzi wa elimu ya juu, uhakiki wa vyeti vya watumishi wa umma, uboreshaji wa Sheria ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HELSB), uhakiki wa wanafunzi hewa na kuzidhibiti shule binafsi kuchuja wanafunzi.

Hata hivyo, ugumu unaomkabili Prof. Ndalichako na msaidizi wake, Mhandisi Manyanya katika utekelezaji wa bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka huu wa fedha, ni kutoa ajira kwa walimu na kuboresha mazingira ya ujifunzaji na ufundishaji.

Ili kukwepa kushukiwa na wabunge wakati vikao vya Bunge la Bajeti ya pili ya serikali chini ya Rais John Magufuli, vitakavyoanza Aprili 4, mawaziri hao pia wanapaswa kuandaa maelezo ya kina kuhusu kitendo cha wizara sita kuweka ofisi kwenye Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom).

Ikiwa imebaki takribani miezi minne mwaka wa bajeti kufika kikomo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imebainisha kuwa mawaziri hao wanakabiliwa na mtihani mgumu kutekeleza majukumu yao na bajeti ya wizara yao kutokana na ukata.

Katika mahojino mahususi na Nipashe Februari 25, mwaka huu, Waziri Kivuli wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Suzan Lyimo, alisema utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya wizara hiyo kwa mwaka huu wa fedha unasuasua na kuna hatari miradi mingi kutotekelezeka kutokana na kutopewa fedha zilizoidhinishwa na Bunge.

Lyimo ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), alisema utekelezaji wa bajeti ya wizara hiyo haufiki hata asilimia 50.

"Hoja hapa kwanini serikali haitoi fedha kama tulivyopitisha bungeni. Kazi yangu imekuwa kupigania bajeti ya Wizara ya Elimu iongezeke, lakini hata kidogo tunachoidhinisha, nacho hakitolewi kwa wakati," alisema Lyimo.

Aliongeza: "Utekelezaji wa bajeti ni mbaya sana na ndiyo maana kuna mambo hayaendi vizuri ikiwa ni pamoja na Sera ya Elimu Bure."

Alisema upinzani itashirikiana na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii (Lyimo ni mjumbe wa kamati hiyo), kuibana serikali kuhusu utekelezaji wa bajeti ya wizara hiyo.

UPUNGUFU WA WALIMU
Wakati ajira mpya serikalini zimesitishwa kupisha uhakiki wa watumishi hewa, Prof. Ndalichako na Mhandisi Manyanya, wanatakiwa kuhakikisha wanatatua changamoto ya uhaba wa walimu nchini.

Kwenye ukurasa wa 26 wa kitabu cha bajeti ya wizara yao kwa mwaka huu wa fedha, inaelezwa kuwa hadi Mei 26, mwaka jana, kulikuwa na upungufu wa walimu wa sayansi na hisabati 22,000 nchini.

SERIKALI KUHAMIA UDOM
Mawaziri hao wanatakiwa kujipanga kutoa maelezo ya kina kuhusu sababu za wizara yao kuruhusu wanafunzi wa Udom kuchanganywa na watumishi wa serikali kutoka wizara sita ambazo zimeweka makazi chuoni hapo katika kipindi hiki cha serikali kuhamia mkoani Dodoma.

Ikumbukwe kuwa Februari mosi, mwaka huu, Makamu Mkuu wa Udom, Prof. Idris Kikula, alisema wizara sita zitaweka makazi yake chuoni hapo huku akidai haoni tatizo kwa serikali kuweka makazi yake hapo.

Kwa mujibu wa Prof. Kikula, wizara ambazo zimeweka makazi Udom ni Katiba na Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Viwanda na Biashara, Afya, Elimu na Mambo ya Ndani ya Nchi.

Februari 6, mwaka huu, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, ilipokuwa inawasilisha bungeni taarifa ya utekelezaji wa majukumu yake, ilipinga uamuzi wa wizara kuweka makazi Udom ikitahadharisha kuwa utaratibu huo ni hatari kwa maendeleo ya wanafunzi.

"Kamati inaunga mkono mpango wa serikali kuhamia Dodoma, lakini utaratibu wa wizara kuhamishia ofisi zao katika Chuo Kikuu cha Dodoma si sawa," Peter Serukamba, Mwenyekiti wa kamati hiyo, aliliambia Bunge siku hiyo.

Aliongeza: "Kamati inaona kuna bomu kubwa linakuja kulipuka kwa kuwachanganya wanafunzi na wafanyakazi kwani kutasababisha wanafunzi wasijikite katika masomo."

Alisema kamati yake inashauri serikali itafute majengo mengine ikiwezekana kujenga majengo kwa shughuli za ofisi za serikali na siyo Udom kwa kuwa lengo lake tangu mwanzo halikuwa kukifanya chuo hicho kuwa ofisi za wizara.

PIKIPIKI MIKOA 18
Kwenye ukurasa wa 20 wa kitabu cha bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa mwaka huu wa fedha, inaelezwa kuwa wizara hiyo inatakiwa kuhakikisha inanunua na kugawa pikipiki kwa waratibu elimu kata wa mikoa 18 na kuchangia mafuta kwa ajili ya magari na pikipiki zilizonunuliwa chini ya Mpango wa Kukuza Stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (Lanes).

UKARABATI SHULE KONGWE.
Ili kukwepa kibano cha wabunge kwa kuwasilisha bajeti 'hewa' bungeni, mawaziri hao pia wanatakiwa kutekeleza ukarakabati wa shule kongwe za sekondari 33 kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji.

Shule hizo kwa mujibu wa kitabu cha bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka huu wa fedha ukurasa wa 28 ni pamoja na Ilboru, Kilakala, Mwenge, Msalato, Mzumbe, Nganza, Pugu, Same, Tabora Boys na Tabora Girls.

Nyingine ni Azania, Jangwani, Kantalamba, Mpwapwa, Tosamaganga, Malangali, Milambo, Nangwa, Kibiti, Minaki, Ifakara, Songea Boys, Ndanda, Kigoma, Kibaha na Ihungo ambayo hata hivyo, tayari imekarabatiwa kwa fedha zilizotokana na michango ya wadau kusaidia waathirika wa tetemeko la ardhi lililoikumba Kanda ya Ziwa Septemba 10, mwaka jana na kuuathiri zaidi mkoa wa Kagera.

Shule nyingine ni za ufundi za Bwiru Boys, Ifunda, Iyunga, Moshi, Mtwara, Musoma na Tanga.

NYUMBA ZA WALIMU
Mawaziri hao pia wanatakiwa kuwezesha ujenzi wa nyumba 30 za walimu zenye uwezo wa kuchukua walimu 180 kwenye maeneo yasiyofikiwa kirahisi. Pia kuwezesha ujenzi wa vyumba 25 vya madarasa na matundu 200 ya vyoo katika shule zenye uhitaji mkubwa.

Katika mwaka huu wa fedha, mawaziri hao pia wanatakiwa kuhakikisha wanaanza ujenzi wa Kituo Mahiri cha Magonjwa ya Moyo na Mishipa ya Damu cha Afrika Mashariki kwenye eneo la Mlongazila jijini Dar es Salaam.

UDHIBITI WA MIONZI
Prof. Ndalichako na Mhandisi Manyanya pia wanatakiwa kuhakikisha wananchi na viumbe hai hawaathiriwi na mionzi hatarishi hasa kwenye sehemu za kazi kwa kufanya ukaguzi wa migodi mitano mikubwa inayofanya kazi ili kubaini hali ya usalama inayoendelea katika migodi hiyo.

Pia wanatakiwa kuhakikisha vituo 120 vyenye vyanzo vya mionzi vinakaguliwa ili kubaini hali ya usalama kwa wafanyakazi 1,700 na umma kwa ujumla.

VYUO VYA UFUNDI
Mawaziri hao pia wanatakiwa kujenga vyuo vipya vya ufundi katika Wilaya ya Chato na Nyasa, kujenga bweni la wasichana katika Chuo cha Veta Mbeya na kukamilisha ujenzi wa chuo cha ufundi stadi katika Halmashauri ya Wilaya ya Busokelo.

VIFAA VYA MAABARA
Prof. Ndalichako na Mhandisi Manyanya pia wanatakiwa kuhakikisha shule za sekondari zinakuwa na vifaa vya maabara na vitabu.

Kwenye ukurasa wa 75 wa kitabu chao cha bajeti ya mwaka huu wa fedha, inaelezwa kuwa wizara hiyo inatakiwa kuhakikisha maabara zote zilizojengwa na halmashauri kwa kushirikiana na wananchi zinapatiwa vifaa vya maabara ili elimu itolewe kwa viwango vinavyotakiwa.

MAJI SHULENI
Kabla ya kufika kikomo kwa mwaka wa bajeti, mawaziri hao pia wanatakiwa kuhakikisha mradi wa Huduma ya Maji, Elimu ya Afya na Usafi wa Mazingira (Swash) unatekelezwa katika shule 4,200.

Kwenye ukurasa wa 73 wa kitabu cha bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka huu wa fedha, inaelezwa kuwa kati ya shule hizo zinazopaswa kufikiwa na mradi huo, 3,500 ni za msingi na 700 ni za sekondari.

Usikose kufuatilia uchambuzi huu kesho

Habari Kubwa