Akatwa kwa wembe sehemu za siri na mke wake

09Apr 2020
Marco Maduhu
Shinyanga.
Nipashe
Akatwa kwa wembe sehemu za siri na mke wake

Shaibu Jabuka (36) mkazi wa Ngokolo Manispaa ya Shinyanga, amedaiwa kujeruhiwa na mke wake aliyefahamika kwa jina moja la Mwajuma, kwa kukatwa kwa wembe sehemu za siri eneo la Korodani ya kulia, kwa madai ya kumnyima pesa ya matumizi Shilingi 10,000.

Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga Debora Magiligimba akizungumza na waandishi wa habari.

Akitoa taarifa leo Aprili 9,2020 kwa vyombo vya habari, Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga Debora Magiligimba, wakati akizungumza na waandishi wa habari, amesema tukio hilo limetokea Aprili 6 mwaka huu majira ya saa 7 usiku.

Akisimilia tukio hilo, Kamanda Magiligimba amesema mara baada ya mwanaume huyo kujeruhiwa na mke wake, alikimbizwa katika Hospitali ya Rufani ya mkoani Shinyanga kupatiwa matibabu na amesharuhusiwa, huku mwanamke huyo akikimbia kusikojulikana, ambapo Jeshi hilo linaendelea na juhudi za kumtafuta.

“Chanzo cha tukio hili ni mwanaume kumnyima mke wake pesa ya matumizi Shilingi 10,000, ndipo ukaibuka ugomvi na kusababisha mwanaume kukatwa sehemu zake za siri eneo la Korodani la kulia,” amesema Magiligimba.

“Natoa wito kwa wanandoa au watu wenye mahusiano ya kimapenzi, wanapokuwa na mgogoro waache kuchukuliana sheria za mkononi, bali wapeleke matatizo yao kwa wazee wenye busara au wafike kwenye ofisi za ustawi wa jamii na dawati la jinsia na watoto kutoka Jeshi la Polisi ili kumaliza tofauti zao,” ameongeza 

Katika hatua nyingine amesema Jeshi hilo limefanya msako na doria mbalimbali katika kipindi cha kuanzia Disemba 2019 hadi Machi 2020, na kufanikiwa kukamata watuhumiwa 48 wakiwa na mali mbalimbali zidhaniwazo kuwa za wizi, ambapo 28 kati yao wameshafikishwa mahakamani, huko 20 upelelezi bado unaendelea.

Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga Debora Magiligimba akionyesha mapipa ya kutengenezea pombe aina ya Gongo.
Pikipiki na Baiskeli ambazo zimekamatwa.

Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga Debora Magiligimba akionyesha vitu vya wizi ambavyo wamevikamata katika misako na doria mbalimbali.

Aidha ametaja vitu hivyo kuwa ni Magodoro Nane, Television Tisa, Pikipiki Nne, Baiskeli Tano, Sabufa Tatu, Laptop Nne, Vitenge pea Tisa, Pasi ya umeme moja, Cpu Mbili, King’amuzi kimoja, Mirungi mabunda matatu, Bangi mafurushi matatu na kete 305, mtambo wa kutengeza Gongo, sabuni B29 boksi tatu, Pikipiki Nne, Baiskeli Nne, pamoja na mchele kilo 43.

Pia ametoa wito kwa wananchi mkoani Shinyanga katika kusheherekea siku kuu ya Pasaka, wakae majumbani mwao na kuepuka misongamano ili kuendelea kujikinga na maambukizi ya virusi vya Corona, huku akiwataka madereva wa vyombo vya moto kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kuepusha ajali zisizo za lazima.

Habari Kubwa